emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

​Mifumo ya TEHAMA Kuinua Wananchi


​Mifumo ya TEHAMA Kuinua Wananchi


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius John Ndejembi ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kubuni, kusanifu na kutengeneza mifumo inayosaidia taasisi za umma kutekeleza majukumu yake kwa urahisi na ufanisi zaidi.

Mhe. Ndejembi ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya Ufunguzi wa mauzo ya Vipande vya faida fund na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroni wa Uendeshaji wa mfuko huo iliyofanyika katika Ukumbi wa Kisenga jengo la LAPF Millenium Towers Dar es Salaam Novemba 1, 2022.

“Watumishi Housing Investment na Mamlaka ya Serikali Mtandao ziko chini ya ofisi yangu na zimefanya jambo kubwa la kiubunifu la kutengeneza mfumo mahususi wa pamoja unaohusu masuala ya Uwekezaji. Ubunifu huu unawasadia wananchi wote hususani wa hali ya kati na ya chini kunufaika na huduma za Serikali mtandao mahali na wakati wowote. Hivyo, sisi kama Serikali hatuna budi kutoa pongeza kwa viongozi na watumishi katika ofisi hizi mbili kwa ubunifu wenye tija” Alisema Mhe. Ndejembi.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA-eGA Bw. Ricco Boma amesema kuwa mfumo huu unamwezesha Mwekezaji kuchagua njia mojawapokati ya njia tatu za kutumia kununua au kuuza vipande. Njia ya kwanza ni ya Mtandao (Web Application) kwa kubofya www.fas.whi.go.tz, ya pili ni kwa simu ya kiganjani hususani kwa wawekezaji ambao hawana intaneti. Huduma hii inapatikana wakati na muda wowote kupitia menyu ya Huduma za Serikali ya *152*00#. Endapo mwananchi atabofya namba hiyo atakuwa na uwezo wa kuona orodha ya huduma lakini kwa mantiki hii atachagua namba 1 Malipo, namba 6-WHI kisha kufuata maelekezo.

Njia nyingine ni ya kupakua Faida Fund App, Bw. Ricco ameongeza kuwa njia hii inahitajimwekezaji awe na simu janja yaani smartphone ambapo ataingia Playsore na kutafuta Faida Fund Appkisha atapakua au download na kujaza taarifa zake kwa usahihi hasa namba ya simu au baruapepe yake ili aweze kupokea namba ya malipo atakayotumia kulipa wakati wa kununua vipande na kufuatilia mwenendo wa uwekezaji wako.

“Mfumo huu ni salama kwa kuwa umezingatia viwango vya Kimataifa na vile vya Serikali Mtandao Tanzania. Pia, mfumo ni rahisi kwa kuwa mwekezaji anaweza kununua vipande kwa kutumia control namba moja aliyopewa na habari njema ni kuwa haitakwisha muda wake, hivyo itatumika kipindi chote cha uwekezaji wake” alisisitiza Bw. Ricco.

Katika hafla hiyo, Watumishi Housing Investments imefanya ufunguzi wa mauzo ya vipande vya Faida Fund na kuzindua Mfumo wa Kielektroni wa Uendeshaji wa Faida Fund uliobuniwa na kutengenezwa na Watumishi Housing Investment kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao-eGA kwa lengo la kurahisha utaoji wa huduma kwa wawekezaji. Uzinduzi umefanyika katika Ukumbi wa Kisenga jengo la LAPF Millenium Towers.

Tanzania Census 2022