emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Serikali yahimizwa kuwa na Mfumo wa pamoja


Serikali yahimizwa kuwa na Mfumo wa pamoja


Naibu waziri, ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius John Ndejembi amesema wakati umefika kwa serikali kuwa na mfumo wa pamoja utakaojumuisha huduma zote badala ya kila taasisi ya umma kuwa na mfumo wake ndani ya serikali moja.

Wito huo ameutoa Desemba 31, 2020 wakati alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) zilizopo mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha na kufahamu zaidi shughuli za Taasisi hiyo.

Aidha, amezitaka taasisi za umma kuwa na utayari wa kutumia Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa huduma na ushauri ili Serikali iweze kupata thamani halisi ya uwekezaji katika mifumo na miundombinu ya TEHAMA.

“Taarifa yenu inaonesha kuwa tuna wataalamu wenye weledi wa kutosha kuunganisha huduma zote kwenye mfumo mmoja, hivyo nimatumaini yangu kuwa zoezi hili litafanyika kwa kasi ili kumuwezesha mtumiaji kupata huduma zote mahala pamoja” amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Sambamba na hilo Mhe. Ndejembi ameahidi kushirikiana na e-GA ili kuongeza ufanisi Serikalini hususa ni kwa taasisi za umma kutumia mifumo inayotengenezwa na wataalamu wa ndani ya Serikali. Hatua hiyo itamsaidia Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Kutimiza azma yake ya kurahisisha upatikanaji na utoaji wa huduma kwa wananchi na si vinginevyo.

Pia, Naibu Waziri Ndejembi ameipongeza menejimneti na watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kazi nzuri na kuwataka waongeze juhudi ya kubuni mifumo mbalimbali itakayorahisisha utendaji kazi ndani ya Serikali.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Kuwe Bakari alimuarifu Naibu Waziri huyo kuwa tangu iliyokuwa Wakala ya Serikali Mtandao hadi sasa Mamlaka, imebuni, imesanifu na kutengeneza mifumo mingi inayorahisisha utendaji kazi katika taasisi za umma na Serikali kwa jumla kwa kutumia wataalamu wa ndani. Aidha, kuahidi kufanya kazi kwa bidii, kwa kushirikiana na taasisi nyingine ili ziweze kutoa huduma kwa ufanisi na kwa gharama nafuu.
Tanzania Census 2022