Serikali Yasisitiza Uwekezaji Katika Mafunzo ya Teknolojia kwa Watumishi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuwajengea uwezo watumishi wake katika matumizi ya teknolojia zinazochipukia, ili kuhakikisha zinatumika kwa usalama na kuleta tija inayokusudia.
Mhe. Ridhiwani ametoa rai hiyo Novemba 25 mwaka huu, alipozungumza na watumishi wa e-GA wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dodoma.
Alisema kuwa, teknolojia hukua na kubadilika kila mara hivyo, ni muhimu kwa e-GA kuhakikisha watumishi wake wanapata mafunzo mbalimbali kuhusu teknolojia hizo na kuangalia namna zinavyoweza kutumika na kuleta tija kwa taifa.
“Kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani imeleta mwelekeo mpya katika uongozi na utendaji kazi, sambamba na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Serikali, lakini ili tuweze kutumia teknolojia hizi ni lazima tuwekeze katika kuwajengea uwezo watumishi wetu ili waweze kuangalia namna Tanzania inavyoweza kuzitumia na kunufaika nazo”, alisisitiza Mhe. Ridhiwani.
Aidha, aliongeza kuwa teknolojia ni eneo muhimu ambalo likitumika vizuri litasaidia kupunguza changamoto ya ajira nchini, kwani vijana wengi wanaweza kujiajiri kupitia matumizi ya teknolojia mbalimbali na hivyo kujikwamua kiuchumi.
Alisema, pamoja na matumizi ya teknolojia kuongezeka kwa kasi duniani ni muhimu kama taifa liwe na uratibu mzuri wa teknolojia hizo, ili kuhakikisha zinatumika kwa manufaa na kuleta tija iliyokusudiwa.
“Kadri kasi ya matumizi ya teknolojia yanavyoongezeka hatari za kiusalama nazo zinaongezeka, hivyo e-GA mnao wajibu mkubwa wa kuhakikisha mnaimarisha usalama wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA Serikalini dhidi ya matishio ya usalama wa kimtandao”, aliongeza Mhe. Ridhiwani.
Sambamba na hilo, Mhe. Ridhiwani aliipongeza e-GA kwa kuendelea kuimarisha usalama wa mifumo, na kusisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo watumishi katika usalama wa kimtandao ili kuweza kukabiliana na uhalifu wa kimtandao kadiri teknolojia inavyokua.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Regina Ndege, aliwashukuru watumishi wa e-GA kwa mapokezi mazuri na kuwasihi kuimarisha ushirikiano na Wizara katika utekelezaji wa majukumu yake, ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo ya kuwa na Serikali Mtandao yenye tija.
Aliongeza kuwa, Serikali ya awamu ya sita imejidhatiti katika kuimarisha matumizi ya Serikali Mtandao na kuwa Wizara kupitia e-GA, imepewa jukumu hilo muhimu la kuhakikisha inafikia malengo hayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba, aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano na Wizara sambamba na kutekeleza kwa wakati maelekezo yote yatakayotolewa ili kujenga Serikali Mtandao yenye tija.
Hii ni ziara ya kwanza ya kikazi kwa viongozi hao wa Wizara, tangu kuteuliwa kwao na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka huu.



