Serikali Yazindua Mifumo ya GSD na NGAO Kuimarisha Huduma za Umma

Serikali imezindua mifumo ya Dawati la Huduma za Serikali (Government Service Directory - GSD) na NGAO, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma za umma kwa njia za kidijiti pamoja na kuongeza usalama wa mifumo ya Serikali.
Uzinduzi huo ulifanyika Juni 23, 2026, jijini Dodoma katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, alimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Prof. Shemdoe alisema kuwa, mifumo hiyo ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali katika kuboresha huduma kwa wananchi kupitia teknolojia.
“Mfumo wa GSD utarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za Serikali kupitia dirisha moja, na mfumo wa NGAO utaimarisha usalama wa taarifa za Serikali kwa kutumia uthibitishaji wa vipengele vingi (Multi-Factor Authentication)”, alisema Prof. Shemdoe.
Alibainisha kuwa, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yamekuwa nguzo muhimu katika kuongeza ufanisi wa Serikali kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuimarisha uwazi na kupunguza gharama za utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Katika dunia ya sasa matumizi ya mifumo ni jambo la lazima. Taasisi zote za umma zinapaswa kutumia mifumo ya TEHAMA kwa ufasaha ili kuboresha huduma kwa wananchi na kusimamia vizuri rasilimali watu," alisema Prof. Shemdoe.
Aidha, aliiagiza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kuendelea kusimamia uunganishaji wa mifumo ya Serikali kupitia Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus - GovESB), ili taasisi za umma ziweze kubadilishana taarifa kwa ufanisi, kupunguza urudufu wa taarifa na kuongeza tija katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi, alisema mfumo wa GSD utawarahisishia wananchi kupata huduma zote za Serikali kidijitali kupitia dirisha moja, ikiwa ni pamoja na kuona huduma zinazotolewa, gharama zake, masharti ya kupata huduma na namna ya kuzifikia hata wakiwa nyumbani kwa kutumia anwani za makazi (NAPA).
Alibainisha kuwa, zaidi ya taasisi 500 za umma tayari zimeingiza huduma zao katika mfumo wa GSD na kuzitaka taasisi ambazo bado hazijakamilisha zoezi hilo kufanya hivyo kwa wakati.
Kuhusu mfumo wa NGAO, Bw. Mkomi alisema mfumo huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Usalama wa Serikali Mtandao na Muongozo wa Matumizi Bora, Sahihi na Salama ya Vifaa, Data na Mifumo ya TEHAMA Serikalini wa mwaka 2022, unaolenga kudhibiti matishio ya kimtandao yanayoweza kuathiri utendaji wa Serikali na utoaji wa huduma kwa umma.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yalishirikisha zaidi taasisi 226, zikiwemo Mamlaka, Mashirika ya Umma, Benki na Wizara mbalimbali ambazo zilitoa huduma na elimu mbalimbali kwa wananchi.



