emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Sheria na Kanuni za Serikali Mtandao (Serikali ya Kidigitali) zinasaidia Matumizi Sahihi ya TEHAMA Serikalini


Sheria na Kanuni za Serikali Mtandao (Serikali ya Kidigitali) zinasaidia Matumizi Sahihi ya TEHAMA Serikalini


Taasisi za umma zimeaswa kuzingatia sera, sheria, kanuni, viwango na miongozo ya serikali mtandao wakati wa kusanifu, kujenga na kuendesha mifumo na miundombinu ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.

Hayo, yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari leo Septemba 25, 2020 jijini Dodoma mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 na Kanuni zake za mwaka 2020 kwa Wakuu wa Idara/Vitengo vya TEHAMA Serikalini.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Laurean Ndumbaro katika Ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano ulipo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Aidha, Dkt. Bakari ameeleza kuwa uzingatiaji wa sheria hii na kanuni zake utasaidia kuwezesha matumizi sahihi ya TEHAMA katika taasisi za umma yakayopelekea kuboreka kwa utendaji kazi na kutoa huduma bora zinazopatikana kwa urahisi na haraka, na hivyo kuwa na Serikali ya Kidigitali iliyo imara na endelevu.

“Napenda kuwafahamisha kuwa sheria hii inaelekeza kuwa taasisi za umma zinazohusika na ujenzi wa miundombinu ya Serikali kama vile barabara, reli na majengo kuhakikisha kuwa yanawekewa mazingira wezeshi kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya TEHAMA kuanzia wakati wa kuandaa michoro ya ujenzi wa miundombinu hiyo”.

Pia, Dkt. Bakari amefafanua kuwa taasisi za umma zinatakiwa kuwasilisha mapendekezo na nyaraka zote zinazohusu miradi ya TEHAMA kabla ya kuanza utekelezaji kwa ajili ya kuhakikiwa na kupishwa na Mamlaka, na baadae kuwasilisha taarifa za maendeleo ya utekelezaji, pamoja na taarifa ya mwisho baada ya kukamilika kwa mradi husika.

Aidha, Dkt. Bakari ameongeza kuwa, pamoja na kupitishwa kwa sheria hii, Waziri mwenye dhamana ya kusimamia serikali mtandao ana mamlaka ya kutoa viwango na miongozo kwa ajili ya kusimamia matumizi ya TEHAMA kwenye taasisi za umma, ikiwemo miamala ya kielektroni kwa lengo la kuifanya Serikali kuwa ya Kidigitali zaidi inayo boresha utendaji kazi na utoaji huduma, na kubainisha zaidi kuwa uzingatiaji wake utawezesha kuondoa urudufu na kufanya mifumo ya taasisi za umma kuongea na kubadilidhana taarifa.

“Hivyo basi kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Serikali Mtandao na Kanuni zake, itasaidia kuwa na matumizi sahihi ya TEHAMA miongoni mwa taasisi za umma, hivyo kuwa na utendaji kazi wenye tija na ufanisi na utoaji wa huduma zinazopatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu” alihitimisha Dkt. Bakari.