emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO/IEC 27001:2022 | ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuboresha usimamizi wa shughuli mbalimbali za kilimo nchini.

Akizungumza katika Maonesho ya kitaifa ya wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Meneja Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga, amesema e-GA imekuwa ikibuni na kusimamia mifumo ya TEHAMA inayosaidia taasisi mbalimbali kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Alitaja baadhi ya mifumo iliyotengenezwa ni pamoja na e-Kilimo unaoiwezesha Wizara ya Kilimo kupata taarifa za wakulima, kusimamia taasisi zilizo chini ya wizara hiyo pamoja na kutoa vibali mbalimbali vya kilimo.

“Pia, tumeshirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kutengeneza Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU), unaoiwezesha Tume kufuatilia utendaji kazi wa vyama hivyo pamoja na kuwawezesha wakulima kufuatilia mauzo ya mazao yao na hivyo kuongeza uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa vyama”, alifafanua Subira.

Ameongeza kuwa, e-GA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA) imetengeneza Mfumo wa Usimamizi wa Mbolea ‘Fertilizer Information System -FIS’, unaowezesha kusimamia wazalishaji, waingizaji na wasambazaji wa mbolea, kufuatilia mwenendo wa soko pamoja na kuhakikisha wauzaji wanazingatia bei elekezi.

Mbali na mifumo hiyo, Bi.Subira amesema, taasisi za sekta ya kilimo zinaendelea kutumia huduma nyingine za e-GA, ikiwemo matumizi ya mfumo wa barua pepe za Serikali (GMS) na Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), ambayo imeongeza ufanisi wa mawasiliano na usimamizi wa shughuli za kila siku ndani ya Taasisi.

Mpangilio