MAMLAKA ya Serikali Mtandao (e-GA), imetoa tuzo mbalimbali kwa Taasisi za Umma zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kuchochea matumizi ya TEHAMA Serikalini.
Tuzo hizo zilitolewa Februari 13 mwaka huu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene (Mb), wakati akifunga Kikao kazi cha 5 cha Serikali Mtandao, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Aidha, tuzo hizo ziligawanywa katika makundi matatu ya utekelezaji wa Serikali Mtandao ambapo kundi la kwanza lilikuwa ni Uzingatiwaji wa Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao (Best Performance in Compliance to e-Government Act, Standards and Guidelines’.
Kundi hili liliangalia maeneo mawili ambayo ni Taasisi zilizopo katika ngazi ya NNE ya Ukomavu wa TEHAMA Serikalini (Level 4 of e-Government Capability Maturity) na Taasisi zilizopo katika ngazi ya TATU ya Ukomavu wa TEHAMA Serikalini (Level 3 of e-Government Capability Maturity Framework)
Katika ngazi ya NNE ya Ukomavu wa TEHAMA Serikalini, taasisi nne ziliibuka na ushindi ambazo ni Wizara ya Katiba na Sheria ikishika nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) mshindi wa pili, Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) mshindi wa tatu na Mamlaka ya Bandari (TPA) mshindi wa nne.
Aidha, kwa upande wa Taasisi zilizo katika ngazi ya TATU ya Ukomavu wa TEHAMA Serikalini, Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliibuka mshindi wa pekee.
Kundi la pili ni Taasisi Hodari kwenye Matumizi ya TEHAMA katika kuwashirikisha Wananchi (Best Performance in Utilization of ICT for Citizen Engagement), washindi wa kundi hili walikuwa ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo iliibuka kinara kwa kushika nafasi ya kwanza, huku nafasi ya pili ikishikwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) ikishika nafasi ya tatu.
Kundi la tatu lilihusu Taasisi Kinara katika Kuunganisha na Kubadilishana Taarifa, kupitia Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Government Enterprise Servise Bus – GoVESB) ambapo Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) liliibuka na ushindi wa pekee.
Washindi wa tuzo hizo wameipongeza e-GA kwa uandaaji wa tuzo hizo, kwakuwa zinatoa hamasa na ushindani chanya wa matumizi ya TEHAMA Serikalini, hali ambayo inasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Tunaishukuru e-GA kwa kuandaa tuzo hizi kwani zitasaidia kuchochea uzingatiaji wa Sheria ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma.” Alisema, Bw. Plasduce Mbossa,Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari.
Bw. Mbossa ameongeza kuwa tuzo hizo zitaimarisha jitihada zilizopo za Bandari katika kufuata Miongozo mbalimbali ya Serikali Mtandao, katika uendeshaji na usimamizi wa mifumo ya TEHAMA bandarini.
Aidha, Meneja wa Usimamizi wa Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao wa e-GA Bi. Sultana Seiff, alibainisha vigezo mbalimbali vilivyotumika katika ushindani katika kundi la kwanza kuwa ni maeneo mawili ambayo ni Taasisi zilizopo katika ngazi ya NNE ya Ukomavu wa TEHAMA Serikalini, na Taasisi zilizopo katika ngazi ya TATU ya Ukomavu wa TEHAMA Serikalini.
Bi. Sultana alisema kuwa katika kundi la pili la Taasisi Hodari kwenye Matumizi ya TEHAMA katika kuwashirikisha Wananchi, vigezo vilivyoangaliwa ni pamoja na Taasisi zilizounganishwa na Mfumo wa Kutuma, Kupokea na Kufuatilia Malalamiko, Mapendekezo, Maulizo na Pongezi (e-Mrejesho), Idadi ya malalamiko yaliyopokelewa na Taasisi zinazotumia mfumo huo, alama za ushughulikiaji wa malalamiko inayohusisha idadi ya malalamiko yaliyofungwa na idadi ya malalamiko yanayoendelea kushughulikiwa.
Vilevile Bi. Sultana alisema katika kundi la tatu, Mamlaka iliangalia Taasisi zinazobadilishana taarifa kupitia Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (GovESB), tarehe ya kujiunga na mfumo huo, idadi ya maombi ya maunganisho yaliyopokelewa na Taasisi husika, muda unaotumika kuidhinisha maombi ya maunganisho kutoka Taasisi mbalimbali na asilimia ya miamala ya ubadilishanaji taarifa iliyofanyika kikamilifu.
Bi. Sultana ametoa rai kwa Taasisi zote za Umma kuongeza jitihada katika uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao ili kuwezesha matumizi sahihi ya TEHAMA katika taasisi zao yatakayoleta tija katika utendaji kazi.
“Ni matumaini yangu kuwa Taasisi za umma zitaiga mfano wa Taasisi zilizofanya vizuri katika maeneo mbalimbali, yaliyoshindanishwa na mwakani tunatarajia idadi ya Tuzo zitaongezeka,” alisema Bi. Sultana