emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

​TAASISI ZA UMMA ZAHIMIZWA KUTUMIA GovESB


​TAASISI ZA UMMA ZAHIMIZWA KUTUMIA GovESB


Kifungu cha 48 (2) cha Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019, kinaitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao kuanzisha na kuendesha Mfumo wa unaowezesha Mifumo ya TEHAMA Serikalini kuwasiliana na kubadilishana taarifa.

Katika utekelezaji wa matakwa ya kisheria, e-GA imesanifu, kutengeneza na kusimamia mfumo unaowezesha Mifumo ya serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa unaojulikana kama Government Enterprise Service Bus (GovESB).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi. Benedict Ndomba amesema kuwa, awali Taasisi za Umma zilitengeneza mifumo mbalimbali ambayo haikuwa na uwezo wa kuwasiliana na kubadilishana taarifa.

Mhandisi Ndomba ameeleza kuwa, e-GA imetengeneza Mfumo wa GovESB ili kuwezesha mifumo hiyo kubadilishana taarifa kwa wakati ili kupunguza adha kwa wananchi katika upatikanaji wa huduma.

“Mfumo huu unarahisisha utoaji wa huduma kwa mwananchi kwa kuwa taarifa zote zinapatikana katika dirisha moja na zinavutwa kutoka Taasisi moja hadi nyingine kutokana na makubaliano ya Taasisi hizo kulingana na huduma na mahitaji” amesema Mhandisi. Ndomba.

Baadhi ya Taasisi ambazo zimeunganishwa katika Mfumo huu ni pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mahakama, Mamlaka za Bima, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, Mhandisi. Ndomba ametoa wito kwa Taasisi za Umma kuwasilisha makubaliano yao na Taasisi wanazotaka kubadilishana taarifa ili Mamlaka iwasaidie kuunganisha Mifumo yao ili kupata taarifa kwa urahisi pamoja na kuokoa muda na gharama.

Naye, Kaimu Meneja wa Usimamizi wa Ujenzi wa Mifumo ya TEHAMA e-GA Bw. Donald Samwel amesema kuwa GovESB inalenga kutatua changamoto za ubadilishanaji wa taarifa kutoka mfumo moja hadi mwingine Serikalini.