emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TAASISI ZA UMMA ZAIDI YA 80 ZIMEJIUNGA NA MFUMO WA KUBADILISHANA TAARIFA (GovESB)


TAASISI ZA UMMA ZAIDI YA 80 ZIMEJIUNGA NA MFUMO WA KUBADILISHANA TAARIFA (GovESB)


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mha. Benedict Ndomba, amesema kuwa zaidi ya taasisi za umma 80 zimejiunga katika Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus-GovESB).

Ndomba alisema hayo wakati aliposhiriki mahojiano katika kipindi cha Adhuhuri lounge cha UTV Septemba 18, kuhusu jitihada za Mamlaka katika kuhakikisha mifumo ya TEHAMA Serikalini inawasiliana na kubadilishana taarifa.

“Kuanzia mwaka 2021, Mamlaka ya Serikali Mtandao imekuwa ikifanyia kazi mfumo maalumu wa kuwezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa, mfumo huu umekamilika na unatumika, nimatarajio yetu hadi kufikia mwezi Disemba taasisi nyingi zaidi zitakuwa zimejiunga na mfumo huu”, alieleza Ndomba.

Alibainisha kuwa, awali mifumo ya taasisi za Serikali ilishindwa kuwasiliana na kubadilishana taarifa kutokana na kutokuwepo kwa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo inayoweka msingi bora wa utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao. Baada ya uwepo wa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019 mifumo inajengwa kwa kufuata viwango na miongozo, hivyo ni rahisi mifumo hiyo kuunganishwa na kubadilishana taarifa, alifafanua.

“Ili kuwezesha mifumo ya zamani ambayo haikufuata viwango na miongozo kubadilishana taarifa kati yao na ile iliyofuata viwango, Mamlaka imebuni na kujenga mfumo wa GovESB unaowezesha mifumo hiyo kubadilishana taarifa, hivyo kuleta suluhisho la changamoto ya mifumo kutokuwasiliana na kubadilishana taarifa”, alisema Ndomba.

Ndomba ameeleza kuwa matarajio ya Serikali ni kuona Taasisi zote za umma zinazohitaji kubadilishana taarifa zinajiunga katika mfumo huo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mh.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma inawasiliana na kubadilishana taarifa.