emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TASISI MBALIMBALI ZA UMMA ZAFUNGA HESABU KWA KUTUMIA MFUMO WA ERMS


TASISI MBALIMBALI ZA UMMA ZAFUNGA HESABU KWA KUTUMIA MFUMO WA ERMS


Tasisi mbalimbali za Umma zimefanikiwa kuandaa na kufunga hesabu kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa kutumia Mfumo wa kusimamia shughuli na Rasilimali za Tasisi (ERMS).

Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa Utengenezaji wa Mifumo ya Mamlaka Bw. Donald Samwel wakati wa mahojiano na mwandishi wetu ofisini kwake jijini Dodoma, wakati akieleza mafanikio ya Mfumo wa ERMS kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Bw. Donald amezitaja Tasisi hizo kuwa ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Nchini (NBAA), Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TCAA), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).

Aidha, Bw. Donald amefafanua kuwa, ufungaji wa hesabu kwa kutumia Mfumo wa ERMS ni rahisi na una faida nyingi ikiwa ni pamoja na kurahisisha mchakato wa kufanya hesabu, upatikanaji wa taarifa zote za msingi kwa ajili ya kufanya hesabu na kufanya masahihisho ya taarifa husika kwa urahisi.

“Mfumo unaongeza uwazi wa taarifa za fedha zinazowekwa kwenye Mfumo na kuwasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini pia Mfumo huu unazuia mianya ya kughushi taarifa, hivyo taarifa zinazowekwa kwenye Mfumo ni sahihi’’Aliongeza Bw. Donald

Mfumo wa ERMS ulitengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa lengo la kusimamia shughuli za ndani ya Tasisi ili kuboresha utendaji kazi, kusimamia matumizi mazuri ya rasilimali na kuweza kubadilishana taarifa miongoni mwa Idara/vitengo ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za uendeshaji na kutoa huduma bora.

Mfumo huo una moduli zaidi ya 20 zinazowasiliana na kuunganisha shughuli za Idara na vitengo ambapo mpaka sasa unatumiwa na Tasisi zaidi ya 35.