emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tumieni Wataalamu wa Ndani Kutengeneza Mifumo-Mhandisi Fumbe


Tumieni Wataalamu wa Ndani Kutengeneza Mifumo-Mhandisi Fumbe


Taasisi za Umma nchini wametakiwa kutumia wataalamu wa ndani katika kubuni, kusanifu na kutengeneza mifumo itakayorahisiha utendaji kazi na utoaji huduma kwa umma ili kuleta manufaa kwa Taifa.

Hayo, yameelezwa na Mhandisi, Jeremia Fumbe kutoka Wizara ya Maji Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, wakati wa mafunzo ya namna ya kuutumia mfumo mpya wa pamoja wa utoaji Ankara za Maji (Maji intergrated and unified Billing System) kwa Maafisa mbalimbali kutoka Mamlaka za maji nchini yanayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na kufanyika Mkoani Morogoro kuanzia 10-18 Novemba, 2020.

“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kuagiza mifumo kutoka nje lakini mifumo ile inapokuja kutumika hapa nchini kwa sababu ya mazingira inakuwa ikihitaji gharama nyingine ili kufanya ile mifumo iendane na mazingira yetu, hivyo Wizara na Taasisi nyingine iige Wizara ya Maji na wawasiliane na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ili waweze kutengenezewa mifumo inayoendana na mahitaji yao”, amesisitiza Mhandisi Fumbe.

Naye Afisa Ankara na Takwimu kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Eliud kitime amesema Mfumo huo unakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza katika mifumo wa awali kwani wamekuwa wakitumia gharama kubwa sana kwa ajili ya matengenezo ya mifumo hiyo.

Vilevile amesema kuwa, mifumo hiyo ilikuwa haina usalama wa kutosha kwa sababu imetengenezwa na watu wa nje ya Serikali lakini kupitia mfumo wa pamoja wa utoaji Ankara za Maji (Maji intergrated and unified Billing System) uliotengenezwa na wataalamu wa ndani ya Serikali utaleta tija zaidi na matokeo chanya kwa watanzania.

“Ningeziomba Taasisi nyingine za Serikali zikiwa zinahitaji kutengenezewa mifumo ziwasiliane na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwani wana wataalamu wa kutosha na waliobobea katika kutengeneza mifumo”, ameeleza Bw. Kitime.

Naye Salome Mtwale ambaye ni Afisa Ankara za Maji kutoka Mamlaka ya Maji Kigoma amesema mafunzo hayo yamekuwa ni mazuri kutokana na kujifunza vitu vingi ambavyo vitawasaidia katika utendaji wao wa kazi na kuwahudumia wananchi.

“Mfumo huu mpya mimi binafsi nimeupenda na kuufurahia sana kwa sababu kulikuwa na vitu vingi ambavyo havikuwepo kwenye mifumo ya zamani, kwakweli naishukuru sana e-GA kututengenezea mfumo huu utakaotumika na Mamlaka zote za Maji hapa nchini”, amefafanua Bi Salome.

Aidha Bi. Salome amesema kuwa mfumo umerahisisha maeneo mbalimbali kama vile eneo la Ankara ambalo limeunganishwa na huduma ya simu ya mkononi katika kurekodi Ankara na kuingiza kwenye mfumo moja kwa moja na hivyo inaokoa muda.

Naye Bw. Rodgers Kahimba, Mhasibu Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Muleba amesema kuna utofauti mkubwa sana katika mfumo huu mpya ukilinganisha na mifumo ya awali kwani kwa sasa makusanyo yataongezeka maradufu na itaboresha huduma ya maji kwa wananchi

Aprili Mosi mwaka 2019 Wizara ya Maji iliingia Mkataba na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kutengeneza mfumo ambapo Aprili hadi Juni 2020 jumla ya Mamlaka tano zilianza kutumia mfumo huo kwa hatua ya Majaribio. Mafanikio yaliyopatikana kumeifanya Wizara kutoa mafunzo kwa taasisi zote za Maji zilizo chini yake ili kuanza kutumia mfumo huo.