Ufunguzi rasmi wa programu ya Mafunzo kwa Vitendo kwa mwaka 2025 Dodoma.

Programu ya Mafunzo kwa Vitendo inayoratibiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kupitia Kituo chake cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao kwa mwaka 2025 imezinduliwa rasmi jijini Dodoma.
Programu hiyo ya wiki 10 hutolewa kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanaosomea fani ya TEHAMA, ambapo jumla ya wanafunzi 57 wanaosoma fani hiyo kutoka katika Vyuo 13 vya ndani pamoja na chuo kimoja kutoka nje ya nchi, wanashiriki katika programu hiyo.
Akizungumza katika ufunguzi wa programu hiyo tarehe Agosti 02 mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba amebainisha kwamba, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanapata uzoefu na picha pana ya uwiano kati ya kile wanachosoma darasani na uhalisia katika sehemu za kazi.
“Katika mafunzo haya tunahakikisha tunawapa uzoefu na kuweza kubaini juu ya uhusiano uliopo kati ya elimu ya darasani, na soko la dunia ili kuandaa taifa la leo na kesho linaloweza kushindana katika uchumi wa kidigiti”, alifafanua Ndomba.
Kwa upande wake Meneja wa Sheria wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Rafael Rutahiwa, amewasihi wanafunzi hao kuishi katika misingi uadilifu, weled na kuheshimiana wakati wote wakiwa kituoni hapo.
Alifafanua kuwa, uadilifu na weledi hutengeneza mazingira rafiki ya ubunifu na tafiti zenye tija kwa taifa na hatimaye kuleta majibu kwa changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii kupitia TEHAMA.
“Uadilifu na weledi vinahitajika kwa pamoja, kwakuwa mmetoka katika mazingira ya vyuo mbalimbali hivyo kuheshimiana ni jambo muhimu pia, ili muweze kufanya kazi pamoja na kuelewana kwani, kipaji pekee hakiwezi kukupa matokeo chanya kama hautoweza kuishi kwenye misingi hiyo mikuu”, alisisitiza SACP Rutahiwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshi wa mamlaka ya Serikali Mtandao Bi.Stara Kavira, aliwataka wanafunzi hao kujikita katika kubuni mifumo itakayotatua changamoto kulingana na mazingira ya Watanzania.
“Lengo la Mafunzo haya ni kuwapa ujuzi na kuongeza uwezo wa kujenga mifumo kulingana na mazingira yetu ya kitanzania, hivyo mtumie muda wenu vizuri ili kuleta ufumbuzi wa changamoto zetu”, alibainisha Bi.Starah.
Kwa upande wao wanafunzi waliojiunga na programu hiyo wameridhishwa na uwazi pamoja na mfumo uliotumika kutoa nafasi kwa vijana wa vyuo mbalimbali nchini, na kuishukuru Serikali kupitia e-GA kwa kuanzisha programu hiyo.
Wakizungumza baada ya ufunguzi, Amina Kalonge mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoka chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Leticia Omary kutoka Chuo cha Sayansi Mbeya (MUST) wameshauri wanafunzi hasa wasichana kuomba nafasi hizo zinapotangazwa, ili kupata jukwaa la kuwajengea ujuzi na uzoefu katika sekta ya TEHAMA.
Katika mafunzo ya mwaka huu, e-GA imeweka maeneo ya kipaumbele ili kuwawezesha wanafunzi kujikita katika bunifu na tafiti zinazohusu teknolojia za 'Internet of Things - IoT, ‘Blockchain’, Crypocurrency, Machine Learning, Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) na teknolojia ya Usalama wa mifumo ya mtandao.