emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

UJAZAJI NA UTENGENEZAJI WA DODOSO SASA NI KIDIJITALI


UJAZAJI NA UTENGENEZAJI WA DODOSO SASA NI KIDIJITALI


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imefanikiwa kutengeneza mfumo shirikishi wa kidijitali wenye usalama na gharama nafuu unaomuwezesha mwananchi au taasisi kutengeneza na kujaza dodoso, kupata tathmini pamoja na takwimu za dodoso kwa njia ya mtandao.

Hayo yalibainishwa na Meneja wa Kituo cha Utafiti na Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) cha e-GA, Mhandisi Dkt. Jaha Mvulla alipofanya mazungumzo na mwandishi wetu ofisini kwake Jijini Dodoma.

“Mamlaka tuliamua kutengeneza mfumo huu ili kuwepo na mfumo shirikishi na salama wa kuhifadhi takwimu zinazotokana na madodoso, kuzuia urudufu wa utengenezaji wa madodoso, pamoja na kupunguza gharama kutoka kwenye mifumo ya dodoso inayotumia leseni” alisema Dkt. Jaha.

Alifafanua kuwa, mfumo huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni dodoso LITE na dodoso PRO ambapo, katika utengenezaji wa maswali na upatikanaji wa takwimu katika dodoso LITE umefanywa kuwa urahisi zaidi ili kumrahisishia mtumiaji katika kujaza au kutengeneza dodoso.

Walengwa wakuu wa mfumo huu ni Taasisi za Umma na wananchi wenye uhitaji wa kutengeneza madodoso ili waweze kupata takwimu au majibu sahihi ya dodoso husika, alisema Jaha.

“Mfumo huu una uwezo wa kuhifadhi data pia ni salama kwakuwa umejengwa na wataalamu wazalendo wa ndani na unawaruhusu watumishi kufanya uchambuzi, kuhifadhi na kupata takwimu za madodoso ya taasisi yanayotengenezwa, pia taasisi au mtu binafsi anaweza kutengeneza dodoso muda wowote na mahali popote kwa jia ya mtandao” alisema Jaha.

Aidha, mtumishi anaweza kutengeneza dodoso la taasisi na kugawa namba ya dodoso na nywila kwa wahusika tu ili waweze kujaza na pia, mfumo unaruhusu na kuziwezesha taasisi kutengeneza maswali katika fomati mbalimbali na kutumia njia ya program ya simu au Kivinjari katika kujaza dodoso.

Kwa sasa Mfumo huu unapatikana bila gharama yoyote kupitia https://edodoso.gov.go.tz, ili taasisi iweze kuunganishwa na kutumia mfumo huu, taasisi husika inapaswa kuwasiliana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kupitia Dawati la Msaada http://helpdesk.ega.go.tz/.