emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WACHAMBUZI WA MIFUMO WAASWA KUONGEZA WELEDI NA UFANISI


WACHAMBUZI WA MIFUMO WAASWA KUONGEZA WELEDI NA UFANISI


Na. Benchine Bago

Wachambuzi wa Mifumo ya TEHAMA wa taasisi za umma, wameaswa kuongeza weledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuepuka makosa yanayoweza kuisababishia hasara serikali.

Rai hiyo imetolewa Aprili 18, mwaka huu na Afisa TEHAMA Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Joan Valentine, wakati wa kuhitimisha mafunzo maalum ya siku tano kwa Wachambuzi wa Mifumo ya TEHAMA (Certified Business Analysis Professional) yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Alisema kuwa, katika hatua za awali za ukusanyaji wa mahitaji ya mifumo ya TEHAMA wataalamu hao wanapaswa kuzingatia weledi na umakini, ili kutengeneza mifumo ya TEHAMA itakayoweza kutatua changamoto zilizopo, na kuiwezesha serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Makosa madogo katika hatua awali za miradi ya TEHAMA yanaweza kuathiri utekelezaji mzima wa mfumo na kuleta hasara kwa serikali, sisi wataalamu tunaoshiriki hatua za awali za ukusanyaji wa mahitaji, ni muhimu tuzingatie weledi na uadilifu,” alisema Bi. Joan.

Alibainisha kuwa, serikali inawekeza rasilimali nyingi katika utekelezaji wa mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo ni wajibu wa kila mtaalamu kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta tija iliyokusudiwa.

Alifafanua kuwa, wachambuzi wa mifumo ya TEHAMA wanayo nafasi kubwa ya kuzisaidia taasisi za umma kuondoa kasoro mbalimbali za mifumo ya TEHAMA ya taasisi katika hatua za mwanzo za ujenzi wa mifumo hiyo.

“Wajenzi wa Mifumo ya TEHAMA (Developers of ICT systems), hujenga mifumo kutokana na mahitaji yaliyochakatwa na Wachambuzi wa Mifumo, hivyo ikiwa Wachambuzi hao watafanya kazi zao kwa weledi na umakini zaidi, watasaidia kuondoa dosari (weak point) katika mifumo,” alifafanua Bi.Joan.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo Wachambuzi wa Mifumo ya TEHAMA katika kuchambua mahitaji ya watumiaji wa mifumo na kuandaa nyaraka sahihi za miradi ya TEHAMA kabla ya utekelezaji wake.

Mchambuzi Mkuu wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Bi. Kissa Tuntufye, ameishukuru e-GA kwa kuratibu mafunzo hayo kwani yamewaongezea ujuzi katika utekelezaji majukumu yao ya kila siku, wakiwa kama daraja kati ya Wajenzi wa Mifumo na watumiaji wa mifumi ya TEHAMA.

“Ni muhimu kupata mafunzo kama haya ambayo yanatuongezea maarifa ya namna bora ya kuanglia changamoto na kuja na ufumbuzi ambao, tukiwapelekea Wajenzi wa mifumo watajenga mifumo bora ya TEHAMA na kurahisisha utoaji wa huduma za serikali kwa njia ya kidijitali,” alisema Bi.Kissa.

Naye Bi.Leah Makuya ambaye ni Mchambuzi wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Wizara ya Fedha alisema, mafunzo hayo yatachangia katika maendeleo ya Serikali Mtandao kwa kuhakikisha kwamba mifumo inayotengenezwa inatoa majibu kwa changamoto zinazowakabili wananchi.

“Kupitia mafunzo haya, tumepata fursa ya kujifunza mbinu bora za uchambuzi wa biashara (business analysis) na namna ya kuepuka makosa ya kiufundi, ambayo yanaweza kusababisha ucheleweshaji au upotevu wa rasilimali za serikali kwenye Miradi ya TEHAMA,” alisema Bi. Leah.

Mafunzo hayo yaliyotolewa na kampuni ya kimataifa ya Koenig Solutions chini ya uratibu wa e-GA, yalihudhuriwa na washiriki kutoka katika taasisi mbalimbali za umma zikiwemo e-GA, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wizara ya Ardhi, Wizara ya Fedha, pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati ya e-GA ya kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA Serikalini, ili kuwa na ujuzi wa kisasa zaidi kadri mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanavyojitokeza kwa kuzingatia sheria zilizopo.