Wadau wajadili Rasimu ya Matumizi Salama ya Teknolojia Zinazochipukia

Wadau wa Serikali Mtandao kutoka taasisi mbalimbali za umma wamekutana leo jijini Dodoma kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao. Rasimu hiyo inalenga kuimarisha matumizi salama na yenye tija ya teknolojia zinazochipukia (emerging technologies) katika utoaji wa huduma za umma, sambamba na kuboresha usalama wa mifumo na taarifa za Serikali.

Kikao kazi hicho cha siku mbili, kinachoendelea kuanzia Julai 16 hadi 17, 2026, kimeandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa lengo la kukusanya maoni ya wadau yatakayosaidia kuboresha rasimu za viwango na miongozo hiyo kabla ya kuidhinishwa.
Miongoni mwa teknolojia zinazojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na Blockchain, Internet of Things (IoT), Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), Robotics, Virtual Reality – VR, Augmented Reality – AR, Quantum Computing, Advanced Automation zinazochochea mageuzi ya kidijitali na kubadilisha namna taasisi za umma zinavyobuni na kutoa huduma kwa wananchi.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Udhibiti na Usalama wa TEHAMA Ndugu Sylivester Shayo alisema, maendeleo ya teknolojia yanahitaji Serikali kuwa na viwango na miongozo itakayowezesha matumizi yake kwa usalama, ubora na kuzingatia maslahi ya wananchi pamoja na taasisi za umma.
Alieleza kuwa, ushiriki wa wadau mbalimbali katika kupitia rasimu hizo ni muhimu ili kuhakikisha viwango na miongozo itakayopitishwa inakidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye, sambamba na kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Aliongezea kuwa, matumizi ya teknolojia zinazochipukia yana nafasi kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kwa njia za kidijitali, kuongeza uwazi, ufanisi na usalama wa taarifa, hivyo ni muhimu kuweka mazingira madhubuti ya usimamizi wake kupitia viwango vinavyokubalika kitaifa.
“Teknolojia hizi zinatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma katika taasisi za umma, na hivyo kuifanya Serikali kuandaa viwango na miongozo itakayosimamia matumizi yake kwa usahihi na kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa”, alisema Bw. Shayo
Aidha, alisema Mamlaka ina wajibu wa kuhakikisha kuwa matumizi ya teknolojia yanaongozwa na viwango na miongozo madhubuti itakayohakikisha usalama wa mifumo, ubora wa huduma na ulinganifu wa mifumo ya Serikali.
Naye mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Afisa TEHAMA kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa Ndugu, Adelhelm Oddo ameipongeza Mamlaka kwa hatua kubwa inayofanya katika kuimarisha jitihada za Serikali Mtandao na kwamba, kikao kazi hicho kitasaidia kuhakikisha matumizi ya teknolojia mpya yanafanyika kwa kuzingatia viwango vya kitaifa, usalama wa mifumo na taarifa, pamoja na kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau kutoka Wizara, Taasisi na Mamlaka mbalimbali za umma, zikiwemo Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na taasisi nyingine za Serikali.



