emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Wadau wa Serikali Mtandao kutoka taasisi mbalimbali za umma wamekutana jijini ili kupitia na kujadili maboresho ya Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, hatua inayolenga kuongeza tija, usalama na ufanisi katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao nchini.

Wadau hao wamekutana katika kikao kazi kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ili kufanya mapitio ya pamoja, kutoa maoni kuhusu miongozo ya Serikali Mtandao, na kufanya maboresho ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani.

Akifungua kikao hicho, Meneja wa Huduma za Sheria wa e-GA Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Rafael Rutaihwa alisema, maboresho ya viwango na miongozo ya Serikali Mtandao, ni muhimu katika kuimarisha miradi ya TEHAMA Serikalini na kuhakikisha kuwa huduma za kidijitali zinatolewa kwa ubora, usalama na ufanisi unaokidhi mahitaji yaliyopo.

“Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA na mifumo jumuishi ya utoaji huduma, ili mifumo hii ifanye kazi kwa kiwango kinachotakiwa, mapitio ya mara kwa mara ni muhimu katika kuhakikisha miongozo inaendana na mahitaji ya teknolojia ya sasa,” alisema SACP Rutaihwa.

Aidha, alisisitiza kuwa utekelezaji wa miongozo iliyoboreshwa utaongeza uwajibikaji na ulinzi wa mifumo ya Serikali, huku akiwataka washiriki kutengeneza nyaraka zinazotekelezeka na zenye manufaa kwa utendaji wa taasisi zao.

Kwa upande wake, Afisa TEHAMA kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Ndugu Adelhelm Oddo, aliipongeza e-GA kwa kuandaa kikao kazi hicho huku akieleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Mamlaka na wadau wake unaongeza umiliki wa nyaraka hizo na kuimarisha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.

Katika kikao hicho, washiriki walipitia maeneo mbalimbali ya miongozo ikiwemo ujenzi, ununuzi, uendeshaji na usimamizi wa mifumo tumizi ya Serikali Mtandao, miongozo ya kujihami dhidi ya majanga ya TEHAMA, pamoja na usimamizi wa vituo vya kuhifadhia mifumo ya utoaji huduma mtandaoni.

Kikao kazi hicho kilichowakutanisha wataalamu wa TEHAMA kutoka taasisi za umma ni sehemu ya juhudi endelevu za e-GA katika kukuza matumizi ya TEHAMA Serikalini na kuimarisha ulinzi wa mifumo ya Serikali kwa ajili ya kutoa huduma bora, salama na zinazokidhi matarajio ya wananchi.

Mpangilio