emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

WAKAGUZI WA NDANI WATAKIWA KUZINGATIA VIWANGO NA MIONGOZO YA SERIKALI MTANDAO KATIKA MIRADI YA TEHAMA


WAKAGUZI WA NDANI WATAKIWA KUZINGATIA VIWANGO NA MIONGOZO YA SERIKALI MTANDAO KATIKA MIRADI YA TEHAMA


Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu za Serikali (IAG) Mwanyika Semroki, amewataka Wakaguzi wa Ndani kuhakikisha Mifumo ya TEHAMA inayoanzishwa katika Taasisi zao inazingatia miongozo na viwango vilivyowekwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).

Mwanyika alitoa kauli hiyo jana wakati akifunga mafunzo maalum ya ukaguzi wa Mifumo na Miradi ya TEHAMA yaliyotolewa kwa Wakaguzi wa Ndani wa halmashauri na Tawala za Mikoa yaliyofanyika kwa siku tano mkoani Morogoro.

“Mnapokwenda kutekeleza majukumu yenu katika Taasisi zenu, lazima muhoji kama Miradi na Mifumo ya TEHAMA pamoja na mahitaji ya mtumiaji (Taasisi) kama yanaendana na viwango na miongozo ya e-GA” alisema.

Mwanyika aliongeza kuwa, Mifumo ya TEHAMA inapaswa kuwa rahisi na rafiki kwa mtumiaji hivyo, kama Mifumo inayotengenezwa katika Taasisi za Umma si rahisi na rafiki kwa watumiaji basi haifai na hivyo inapaswa kuboreshwa.

Aidha, Mwanyika alifafanua kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yatawawezesha Wakaguzi wa Ndani kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuisaidia Serikali kuona thamani halisi ya fedha ilizowekeza katika Miradi na Mifumo ya TEHAMA.

Akitoa ufafanuzi kuhusu maoni yaliyotolewa na washiriki wa mafunzo hayo, Mwanyika alisema kuwa, mafunzo hayo yatakuwa endelevu ili kuhakikisha Wakaguzi wa Ndani katika halmashauri na Tawala za mikoa yote wanapatiwa mafunzo hayo.

Kwa upande wake Meneja Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao Bi. Sultana Seif Alisema kuwa, e-GA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu za Serikali itahakikisha kuwa Wakaguzi wote wa Nadani katika halmashauri na Tawala za Mikoa wanapata mafunzo hayo kabla ya kuisha mwaka wa fedha 2022/2023.

“Kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha, tutahakikisha Wakaguzi wote wa Ndani tunawajengea uwezo wa kukagua Mifumo na Miradi ya TEHAMA ili kuweza kuibua hoja za ukaguzi mapema na kufanyiwa kazi kabla ya Mkaguzi wa nje”, alisema Bi. Sultana.

Akitoa salamu za shukran kwa niaba ya washiriki Mwidikila Lawrence Silanda - Mkaguzi Mķuu wa Ndani Halmashauri ya Sengerema alisema kuwa, Mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu namna ya kufanya ukaguzi katika Mifumo na Miradi ya TEHAMA na kupendekeza mafunzo hayo yawe endelevu kulingana na mabadiliko ya teknolojia yanayoibuka mara kwa mara.

Mafunzo ya ukaguzi wa Mifumo na Miradi ya TEHAMA yalitolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu za Serikali (IAGO) kuanzia Machi 6-10 mkoani Morogoro ambapo yalilenga kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani katika kukagua Mifumo na Miradi ya TEHAMA katika Taasisi zao.