emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wakuu wa Idara/Vitengo Vya TEHAMA Serikalini Wajengewa Uwezo


Wakuu wa Idara/Vitengo Vya TEHAMA Serikalini Wajengewa Uwezo


Taasisi za umma nchini zimetakiwa kuzingatia kikamilifu Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 na Kanuni zake za mwaka 2020 katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao mahala pa kazi.

Hayo, yameelezwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifungua mafunzo kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini yaliyohusu kujenga uelewa katika utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao na Kanuni zake.

ACP Mahumi ameeleza kuwa, Serikali kupitia Tangazo Na. 964 la tarehe 6/12/2019, ilitangaza kuwa tarehe 15 Disemba 2019 ni siku ya kuanza kutumika rasmi kwa Sheria hii ya Serikali Mtandao na Kanuni zake zilizopitishwa mwanzoni mwa mwaka 2020 ambazo nazo zimeanza kutumika katika kutekeleza sheria hii.

“Tambueni kuwa Sheria hii inaweka msingi wa kisheria wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 na kuanzisha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) yenye jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendeleza utekelezaji wa Serikali Mtandao, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma,”

ACP Mahumi amesisitiza. Aidha, ACP Mahumi amesema kuwa mafunzo haya ni moja ya jitihada za kuongeza uelewa wa mambo ya kuzingatia wakati wa kutumia TEHAMA katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa umma, kwa lengo la kuongeza tija na kutoa huduma bora zinazopatikana kwa urahisi.

“Nazipongeza taasisi za umma ambazo zimefanikiwa kuboresha utendaji kazi na kutoa huduma zao kwa umma kwa kutumia TEHAMA, ingawa tunaelewa kumekuwa na changamoto katika eneo hili, kama vile uwepo wa mifumo isiyoongea na urudufu. Hivyo, sheria hii itasaidia kutatua baadhi ya changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Mamlaka ya Serikali Mtandao kutoa viwango na miongozo ya kitaalamu vya serikali mtandao kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa jitihada mbalimbali za serikali mtandao katika taasisi za umma,” ACP Mahumi ameongeza.

ACP Mahumi ameendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia vipengele vyote vinavyohusu usalama wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA kama vilivyoainishwa katika Sheria ya Serikali Mtandao na Kanuni zake. Uzingatiaji huo utahakikisha usalama wa taarifa za Serikali zilizomo katika mifumo na miundombinu ya TEHAMA inayotumika katika taasisi za umma.

Ingawa mafunzo haya yametolewa kwa Wakuu wa Idara/Vitengo vya TEHAMA, ACP Mahumi amewaasa wakuu hao kuhakikisha na wao wanakuwa walimu kwa kusaidia kuwaelewesha watumishi wenzao katika taasisi zao kuifahamu na kuizingatia sheria hii na kanuni zake wakati wa utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.