emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WATAALAMU WA TEHAMA SERIKALINI WAPEWA MAFUNZO YA AKILI MNEMBA NA UCHAMBUZI WA DATA KUBWA.


WATAALAMU WA TEHAMA SERIKALINI WAPEWA MAFUNZO YA AKILI MNEMBA NA UCHAMBUZI WA DATA KUBWA.


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imeratibu na kuendesha mafunzo ya uchambuzi wa Data kubwa ‘Big data analysis’ na Akili Mnemba ‘Artificial intelligence-AI’, kwa wataalam wa TEHAMA kutoka katika Taasisi mbalimbali za Umma, ili kukuza na kuwajengea uelewa wa pamoja kuhusu teknolojia hizo utakaosaidia kukuza ufanisi na kuongeza ubora wa utoaji huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo Machi 23 mwaka huu, Meneja Usimamizi wa Usalama wa TEHAMA (e-GA) Bw.Riziki Majengo alisema, mafunzo hayo yanaendeshwa na e-GA ikiwa ni utekelezaji wa kifungu cha 5(2)(h) cha Sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 ya Mwaka 2019, kinachoielekeza e-GA kuzijengea uwezo Taasisi za Umma katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.

Abainisha kuwa, miongoni mwa faida za mafunzo hayo kwa Taasisi za umma ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kusaidia kuboresha mifumo ya ndani ya nchi kwa kutumia teknolojia hizo.

‘Tayari tuna mifumo na miundombinu mbalimbali ya kukusanya hizi taarifa nyingi, kwahiyo baada ya mafunzo haya tunaenda kuongeza ubora zaidi kwenye mifumo yetu kwa kutumia Akili mnemba ‘Artificial Intelligence’ ili kufanya mashine kufikiria na kufanya maamuzi mengi zaidi ambapo itasaidia kuongeza ufanisi na kupunguza muda wa utoaji huduma kwa wananchi’’, alisema Riziki.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yameendeshwa kwa vitendo Zaidi na hivyo kuwapa washiriki muda wa kutosha wa kujifunza na kuelewa vema kuhusu ‘Big data analysis’ na ‘Artificial Intelligence’ pamoja na matumizi yake katika mazingira na mifumo ya TEHAMA Serikalini.

Aidha, washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza e-GA na kueleza kufurahishwa na mafunzo hayo ambayo yamewajengea uwezo kuhusu matumizi ya teknolojia hizo na kuahidi kutumia elimu waliyopata kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.

Kwa upande wake Afisa TEHAMA kutoka Tume ya Mipango Bw.Godhard Hunja alisema kuwa, mafunzo hayo yataleta tija kubwa katika taasisi yake kwani yatasaidia katika uchambuzi wa takwimu mbalimbali kutoka kwenye taasisi zinazotekeleza miradi ya maendeleo, jambo ambalo litasaidia kupata majibu yenye tija na kuweza kushauri vyema namna ya kuendelea na utekelezaji wa miradi kulingana na takwimu zilizopokelewa.

Naye Meneja wa Oparesheni Kituo cha Taifa cha kuhifadhi Data (NIDC) Bi. Nasra Mugheiry ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kuwakusanya wataalam kutoka taasisi mbalimbali za umma na kuwapa elimu hiyo muhimu ambayo imekuwa ikitumika katika nchi zilizoendelea

‘’Big data analysis na Artificila intelligence hizi ni teknolojia muhimu sana kwa dunia ya sasa na tayari zinatumiwa na nchi zilizoendelea, kwaiyo sisi kupewa mafunzo haya yatakwenda kuongeza motisha na ujuzi kwa wafanyakazi na pia kuiwezesha serikali kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi’’, alisema Nasra.

Mafunzo hayo ni ya awamu ya pili katika mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo awamu ya kwanza ilifanyika Januari 29 hadi Februari 17 mwaka huu na yalihusisha jumla ya wataalamu 20 kutoka katika Taasisi za Umma 10 na awamu ya pili imefanyika Machi 4 hadi 23 mwaka huu na kuhusisha wataalamu 23 kutoka taasisi za umma 15 na hivyo kufanya jumla ya wataalamu waliopatiwa mafunzo hayo kuwa ni 43 kutoka Taasisi za Umma 25, mafunzo hayo yalifanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha mkoani Pwani katika awamu zote mbili.