WATAALAMU WA TEHAMA WATAKIWA KUSIMAMIA VYEMA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZINAZOIBUKIA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amewataka wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuhakikisha wanasimamia ipasavyo utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa kuzingatia matumizi salama, sahihi na yenye kuzingatia matakwa ya kisheria ya teknolojia zinazoibukia.
Mha. Ndomba ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kuhusu Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Usimamizi na Utekelezaji wa Teknolojia Zinazoibukia, ikiwemo Akili Unde (Artificial Intelligence - AI), Block Chain, Internet of Thing yanayofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 02 hadi 06 Novemba 2026.
Amesisitiza kuwa kukua kwa matumizi ya teknolojia zinazoibukia katika utoaji wa huduma za Serikali kunahitaji wataalamu wa TEHAMA kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mifumo ya kisheria, kanuni, viwango na miongozo inayosimamia matumizi ya teknolojia hizo ili kuhakikisha zinatumika kwa uwajibikaji na usalama.
“Ni muhimu kujengeana uwezo na uelewa wa pamoja kuhusu mifumo ya kisheria na miongozo inayosimamia teknolojia hizi ili kuhakikisha matumizi yake yanakuwa sahihi, salama na yenye tija kwa taasisi za umma na wananchi.” Alisisitiza
Aidha, amewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kuongeza uelewa na uwezo utakaowawezesha kuimarisha usimamizi wa rasilimali za TEHAMA, kuandaa nyaraka mbalimbali za TEHAMA na kusimamia matumizi ya teknolojia zinazoibukia katika taasisi zao kwa kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya Serikali Mtandao.

Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Rafael Rutahiwa amesisitiza kuwa mifumo yote inayobuniwa na kutengenezwa kwa kutumia teknolojia zinazoibukia inapaswa kuzingatia taratibu, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha inakuwa salama, inafanya kazi kwa ufanisi na kutoa matokeo yenye tija katika utoaji wa huduma za Serikali.
Akifafanua zaidi, Kamishna Rutahiwa ameeleza kuwa uzingatiaji wa matakwa hayo ni muhimu katika kuhakikisha teknolojia zinazoibukia zinatumika kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika na kusaidia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa mifumo yote inayotengenezwa kwa kutumia teknolojia zinazoibukia inazingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo iliyowekwa na andiko la mradi linawasilishwa Mamlaka ili kuhakikisha usalama, ubora na tija katika utoaji wa huduma za Serikali.” Alisema SACP Rutahiwa
Nae mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Ndugu Alexander Benedicto Afisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe ameishukuru e-GA kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamekuja kwa wakati muafaka kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji na matumizi ya teknolojia zinazochipukia.
Amesema mafunzo hayo yataviwezesha vyuo vikuu kuboresha na kuandaa mitaala inayokidhi mahitaji ya sasa, kwa kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na matumizi sahihi na yenye tija ya teknolojia zinazochipukia.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uwezo wa wataalamu wa TEHAMA katika kusimamia na kutekeleza mifumo ya Serikali Mtandao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo iliyowekwa, hususani katika kipindi hiki ambacho matumizi ya teknolojia mpya yanaendelea kuongezeka.



