Waziri Kikwete Asisitiza Matumizi ya e-Mrejesho, Aipongeza e-GA.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewataka wananchi kuendelea kutumia mfumo wa e-Mrejesho katika kutoa pongezi, malalamiko na maoni kwa taasisi za umma na kisha kupata mrejesho wa utekelezaji.
Akizungumza hivi karibuni na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mhe.Ridhiwani alisema kwamba, utoaji wa maoni ya mara kwa mara ni jambo muhimu katika kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Alibainisha kuwa, mfumo wa e-Mrejesho ni nyenzo muhimu inayowezesha Serikali kupokea taarifa kwa wakati, na kutathmini maeneo yanayohitaji uboreshaji ili kutoa huduma bora.
“Maelekezo ya Mhe.Rais ni kuhakikisha Serikali inaweza kuzungumza na kukutana na wananchi mara kwa mara, kuwasikiliza na kutatua kero zao, hivyo kupitia mifumo kama e-Mrejesho ni njia sahihi kwa wakati tuliopo,” alifafanua Mhe.Kikwete.
Aliongeza kuwa, mfumo wa e-Mrejesho ni rafiki kwa maeneo yote ya mijini na vijinini hata mahali ambapo kuna changamoto ya mtandao wa inteneti, wananchi wanaweza kutumia mfumo huo kupitia simu za mkononi maarufu kiswaswadu kupitia namba ya msimbo *152*00# bila malipo.
Sambamba na hilo alisema kuwa, Serikali inazingati na kuthamini maoni ya wananchi na itaendelea kuyafanyia kazi na kutoa mrejesho kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya dhana pana ya uwazi na uwajibikaji.
Waziri Kikwete pia ametoa wito kwa viongozi wa Serikali katika ngazi zote kuanzia Wizara hadi Serikali za Mitaa kuhakikisha wanaufuatilia kwa karibu maoni yanayowasilishwa na wananchi kupitia mfumo wa e-Mrejesho na kuyafanyia kazi kwa wakati. Hatua hii, itajenga Imani na ari ya wananchi ya kutumia mfumo huo.
Katika hatua nyingine,Waziri Kikwete ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -UTUMISHI katika kusainifu Mfumo wa Daftari la Huduma za Serikali (Tanzania Government Service Directory -TGSD ) ambao utarahisisha utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi.
Amebainisha kwamba, kupitia mfumo huo wa TGSD, mwananchi ataweza kupata taarifa kuhusu utaratibu wa upatikanaji wa huduma za Serikali, gharama zake na vituo ambavyo huduma hiyo inapatikana na njia za mawasiliano.
Mfumo wa TGSD umedhamiria kuongeza ufanisi na uwazi katika utoaji wa huduma zote za Serikali kidijitali.



