emblem
Mamlaka ya Serikali Mtandao
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb), ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa usimamizi mzuri wa taasisi hiyo.

Mhe. Waziri ameyasema hayo Mei 20, mwaka huu wakati alipofanya kikao kazi maalum na bodi hiyo katika ofisi za e-GA Mtumba jijini Dodoma.

Aliongeza kuwa, usimamizi makini wa bodi hiyo umeiwezesha e-GA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo iliyojiwekea kwa wakati.

Ameyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Governement Enterprise Service Bus - GovESB), ambao unaziunganisha na kuziwezesha taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijitali.

“Moja ya mafanikio ya bodi hii ni kusimamia utekelezaji wa agizo la Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha mifumo ya Serikali inawasiliana na kubadilishana taarifa na hili mmelitekeleza kwa kuhakikisha e-GA inajenga mfumo huu wa GoVESB,” alisema Waziri.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na usimamizi wa miundombinu na mifumo ya TEHAMA Serikalini, sambamba na kuimarisha na kudhibiti usalama wa mifumo hiyo.

Waziri alisema, umakini wa bodi hiyo umeiwezesha e-GA kusimamia usalama wa mifumo ya TEHAMA Serikalini jambo ambalo lisingesimamiwa vizuri lingeweza kuleta hatari za kiusalama.

Aliongeza kuwa, usimamizi makini wa bodi na menejimenti ya e-GA umekuwa chachu katika mageuzi ya Serikali Mtandao,  na kuipa nchi heshima kubwa katika anga za kimataifa ikiwemo kupokea tuzo mbalimbali.

“Mwaka 2024 tulishinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Utoaji wa Huduma kwa Umma (UN Public Service Innovation Award) kupitia mfumo wa e-Mrejesho na mwaka huu tumeingia tena katika mashindano ya Tuzo za Dunia za Jumuiya za TEHAMA (World Summit on The Information Society - WSIS), tumechaguliwa kushiriki katika ushindani wa tuzo hizo,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya e-GA Dkt. Mussa Kissaka alimshukuru Mhe. Waziri kwa pongezi na kuahidi kuendelea kuisimamia vizuri e-GA ili iweze kufikia malengo yake.

“Bodi ya wakurugenzi inaahidi kuendelea kuisimamia vizuri e-GA, licha ya mafanikio haya ambayo Mhe. Waziri umeyataja hapa leo, tutaendelea kuisimamia vizuri zaidi e-GA na kuhakikisha inatekeleza majukumu yake na kuendelea kushinda tuzo za kimataifa,” alisema Dkt. Kissaka.

Pamoja na hayo, Dk. Kissaka aliishukuru Menejimenti ya e-GA kwa ushirikiano inaoupata kwakuwa hutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na bodi hiyo kwa wakati.

Mpangilio