emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019. Ni taasisi yenye mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma.

Kuanzishwa kwa Mamlaka hii mwaka 2019 kunaendeleza afua za Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) na kuchukua sehemu ya mipango yake kwa sababu majukumu ya taasisi hizi yanafanana ingawa yanatofautiana katika mamlaka ya utendaji.

Mamlaka ya Serikali Mtandao ni taasisi iliyoirithi Wakala ya Serikali Mtandao iliyoundwa Aprili 2012 kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 Sura ya 245 ya mwaka 1997 yenye jukumu na Mamlaka ya Kuratibu, Kusimamia na Kukuza Jitihada za Serikali Mtandao nchini Tanzania.

Kabla ya kuanzishwa Wakala ya Serikali Mtandao, matumizi ya TEHAMA Serikalini yalikuwa yanaratibiwa na kusimamiwa na Idara ya Usimamizi wa Mifumo (DMIS) iliyopo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambayo kwa sasa ni Idara ya Huduma za TEHAMA Serikalini (DICTS).

Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019 imeainisha majukumu na mamlaka yanayoiongoza Mamlaka ya Serikali Mtandao katika utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini Tanzania.

Dira

Kutambuliwa kuwa taasisi inayoongoza kwa ubunifu katika kuwezesha matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma kwa umma.

Dhamira

Kujenga mazingira wezeshi ya kisheria kwa ajili ya uratibu, usimamiaji na uendelezaji wa matumizi ya TEHAMA ili kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kwa umma.

Kaulimbiu

Uadilifu na ubunifu kwa utoaji wa huduma bora kwa umma.

Misingi Mikuu

Mamlaka inaongozwa na misingi mikuu Sita ambayo inaelekeza kuhusu tabia na mwenendo wa watumishi wake kwa ngazi zote. Misingi hiyo inafafanua utamaduni wa mahali pa kazi, kuhakikisha watumishi wote na wateja wa Mamlaka wana uelewa wa pamoja wa jinsi wanavyotakiwa kuhudumiwa na nini kichotarajiwa kutoka kwao.

Uadilifu

Tunafuata viwango vya uendeshaji vya hali ya juu katika kila tunachofanya kwa kutambua kuwa uhusiano wa kweli na uaminifu ni muhimu kwa mafanikio endelevu ya taasisi.

Ubunifu

Tunazingatia utamaduni wa Mamlaka unaothamini uasili wa uvumbuzi na ubunifu katika kukuza vipaji kwa kuzingatia uwazi na ari.

Kuthamini Wateja

Tunajitoa kwa dhati kuwasaidia wateja wetu wa nje kutimiza malengo yao kwa kuelewa shughuli wanazofanya na kuwapa kile wanachokithamini zaidi.

Kufanyakazi kwa Pamoja

Tumedhamiria kufanya kazi kwa pamoja tukiwa na mawasiliano sahihi ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Ushirikiano

Tunafanya kazi kwa uwazi na taasisi za umma na wadau wengine huku tukibadilishana taarifa, maarifa, uzoefu na tukitambua kuwa tunategemeana kwa maendeleo ya Serikali mtandao.

Weledi

Tunazingatia ubora wa kazi kwa kiwango cha juu na kutoa huduma bora kwa wateja wetu