emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Uzinduzi wa Tovuti za Mikoa na Halmashauri Mjini Dodoma


Uzinduzi wa Tovuti za Mikoa na Halmashauri Mjini Dodoma


“Kwa mara ya kwanza Tanzania Bara imeingia katika historia kubwa Barani Afrika kwa kuzindua Tovuti za Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa 185” Amesema Mhe. George Simbachawene (Mb) ambaye ni mgeni rasmi wa sherehe hizo.

Uzinduzi huo umefanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George Simbachawene (Mb) tarehe 27 Machi, 2017 huko mjini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtanda (eGA) Dkt. Jabiri Bakari na Mkurugenzi Msaidizi wa USAID Tanzania, Bw.Tim Donnay ambao ndio wafadhili wa Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).

Waziri Simbachawene ameshukuru na kupongeza Shirika la Msaada la Watu wa Marekani (USAID) kupitia Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma “PS3”, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wakala ya Serikali Mtandao(eGA) kwa kushirikiana katika kusanifu na kutengeneza mfumo wa pamoja “Government Website Framework” ambao umesaidia kutengeneza tovuti za Serikali zenye kiwango na muonekano mmoja ambao ni rahisi.

“Mfumo huu ni mzuri, rahisi na rafiki kwa waweka taarifa na hata kwa watumiaji. Vilevile kwa kuwa technolojia inabobadilikamara kwa mara ni rahisi kufanya maboresho ya pamoja ya pamoja kwa wakati mmoja” Alisema Simbachawene.

Aidha, Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa suala la upatikanaji habari na taarifa mbalimbali ni takwa la kisheria na kikatiba, hivyo viongozi wa taasisi za umma wana wajibu wa kuhakikisha kuwa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya Serikali zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na tovuti.

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), amesema kuwa tovuti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni njia rahisi na bora ya kuwafikishia wananchi taarifa za utekelezaji Serikalini.

“Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha sheria mbili zinazowapa wananchi haki ya kupata habari na taarifa. Vile vile hakikisheni tovuti zinahuishwa mara kwa mara ili tovuti ziwavutie wananchi wetu” alisema Mwakyembe.

Vilevile Mhe. Mwakyembe, amewataka maofisa Habari na TEHAMA kutambua kuwa wajibu wao ni kuhakikisha tovuti zinapatika wakati wowote na mahali popote zikiwa na taarifa sahihi.

“Ninaomba viongozi wa taasisi za umma kuwapa ushirikiano maofisa habari wanapohitaji taarifa za kuweka kwenye tovuti kwani mafanikio na uhai wa tovuti hutegemea taarifa zinazotolewa na idara na sehemu”. Aliongeza Mwakyembe.

Kwa upande wake,  Mtendaji Mkuu wa eGA Dkt Jabiri Kuwe Bakari amesema hapo awali, Mikoa na Halmashauri nyingi zilikuwa hazina tovuti na zile zilizokuwa na Tovuti, Tovuti hizo hazikufanya kazi vizuri, wakati mwingine hazikupatikana, taarifa zake zilikuwa haziendani na wakati na nyingine zilikuwa na anwani zenye kikoa cha dot.com na hazionyeshi umiliki wa taasisi ya umma. Moja ya hatua za utekelezaji wa Serikali mtandao ni kuwa na uwezo wa kupata taarifa na  huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao kwa urahisi, haraka, gharama nafuu wakati wowote na mahali popote.

Ili kutimiza azma hiyo Dkt. Bakari amefafanua kuwa Maafisa TEHAMA na Maafisa Mawasiliano 422 kutoka katika mikoa na halmashauri hizo wamepata mafunzo ya kutengeneza mwonekano wa tovuti zao na kuweka taarifa kwa ajili ya umma wakiwa mahali popote na wakati wowote kwa kutumia Mfumo wa tovuti tunaouzindua leo.

Aliongeza kuwa Tovuti hizi zitaunganishwa na Tovuti Kuu ya Serikali www.tanzania.go.tz  iliyotengenezwa na Wakala ya Serikali Mtandao na hivi sasa inasimamiwa na kuendeshwa na Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo. Tovuti hii ni dirisha moja la kutolea taarifa na huduma za Serikali kwa umma ambapo kila mwananchi anaweza kuipata wakati wowote  na mahali popote kwa lugha mbili yani ya Kiswahili na Kiingereza.

“eGA imejiandaa vema katika kusimamia na kuhifadhi tovuti zote 211 katika Vituo maalum vya kuhifadhia na kuendesha mifumo mbalimbali ya Serikali Mtandao. Hii itasaidia 3 upatikanaji wa uhakika wa tovuti hizo kwa saa 24 kwa siku 7, badala ya ilivyokuwa hapo awali ambapo kila taasisi ilihifadhi tovuti yake yenyewe na hivyo kusababisha tovuti hiyo kutokuwa hewani endapo hitilafu yoyote itatokea kwenye miundombinu hiyo kama vile kukatika kwa umeme”

Aidha, amezitaka Taasisi za Umma pamoja na wafanyabiashara wanaojihusisha na utoaji wa huduma za TEHAMA katika taasisi za umma wanapaswa kuzingatia miongozo na viwango vya Serikali Mtandao wakati zinapoanzisha miradi yoyote ya TEHAMA. Miongozo na Viwango hivyo vinapatikana katika tovuti ya Wakala ya Serikali Mtandao www.ega.go.tz. Sehemu ya miongozo na viwango.

Jitihada za kutengeneza tovuti hizi zilianza mnamo mwaka 2016 ambapo mikoa ya Mwanza, Dodoma na Iringa ilitumika katika kupata mahitaji ya aina ya tovuti inayotakiwa na mwishoni mwa mwaka 2016 timu ya Watalaam wa eGA, Tamisemi na PS3 ilianza kutengeza mfumo huo ambao umewesha kila Mkoa na halmashauri Tanzania Bara kuwa na tovuti yake.