emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Sefue Kufungua Mkutano wa Serikali Mtandao.


Sefue Kufungua Mkutano wa Serikali Mtandao.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue anatarajia kufungua Mkutano wa Kwanza wa Mwaka wa Serikali Mtandao utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Agosti 2015.

 

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA), Dkt. Jabiri Kuwe Bakari mkutano huo unatarajiwa kuwa na washiriki 500 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Mamlaka, Bodi, Tume, Kampuni za Umma, Mashirika na Mifuko. Wengine wanatoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Mikoa, Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya.

 

Aidha, Dkt. Bakari amebainisha kuwa mkutano huo unalenga kujenga uwezo na ushirikiano kwa watumishi wa umma, kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazokabili jitihada za utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa taasisi za Serikali nchini Tanzania. Pia Mada za Mkutano huo zitajikita katika maeneo ya Sera, Sheria na Miongozo ya TEHAMA, Usimamizi wa matumizi ya TEHAMA, Miundombinu ya TEHAMA, Mifumo Tumizi na Huduma Mtandao kama vile utoaji huduma za Serikali kupitia simu za mkononi pamoja na  Mifumo ya taarifa ya Serikali Mtandao.

 

“Mkutano huu utasaidia kuongeza ufahamu, maarifa na kukuza uhusiano wa kikazi baina ya watalam wetu na wataalam wengine wa Serikali Mtandao kutoka nchi zinazofanya vizuri katika utendaji wa Serikali Mtandao zikiwemo India na Singapore”. Alisema Dkt. Bakari.

 

Vilevile, Dkt. Bakari amesema kuwa viongozi mbalimbali kutoka India na Singapore wamealikwa kushiriki mkutano huo na watapata fursa ya kuwasilisha mada. Viongozi hao ni Dkt. Rajendra Kumar kutoka India na Bw. Tan Kim Leng kutoka Singapore.

 

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala Bi. Suzan Mshakangoto amesema Mkutano huo, unaandaliwa na Wakala ya Serikali Mtandao iliyo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Mkutano huu umegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi kundi la kwanza la tarehe 17 na 18 Agosti 2015 litahusisha Maafisa Tehama, Mipango, Mawasiliano, Utawala na Rasilimaliwatu. Kundi la pili litakutana Agosti 19-20, 2015 na litahusisha viongozi katika ngazi za Makatibu Wakuu, Watendaji Wakuu, Wakurugenzi Wakuu, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mtaa na Wajumbe wa Bodi.

 

Wakala ya Serikali Mtandao ni Taasisi ya Serikali iliyoundwa kwa sheria ya Wakala za Serikali Na. 30, Sura ya 245 ya mwaka 1997. Aidha, imeundwa kama sehemu ya utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa mwaka 2004 kuhusu uanzishwaji wa Serikali Mtandao; na Hati ya Rais ya Mgawanyo wa Majukumu Na. 51 wa tarehe 17 Desemba mwaka 2010 ambao umeipa jukumu na mamlaka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kutayarisha Sera ya Serikali Mtandao na kuhakikisha utekelezaji wake kwa kuanzisha Wakala ya Serikali yenye jukumu na mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao nchini Tanzania. Wakala ilianza kazi ya kutekeleza majukumu yake tarehe 01/04/2012 na kuzinduliwa rasmi mwezi Julai 2012.