emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Uzinduzi wa mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya kuandaa bajeti kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa.


Uzinduzi wa mifumo ya kielektroniki  kwa ajili ya kuandaa  bajeti kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa.


Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amezindua mifumo miwili ya kielektroniki mahususi kwa ajili ya kuandaa  bajeti kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa.

Mifumo iliyozinduliwa ni ule wa Kupanga Mipango, Kuandaa Bajeti na Kutolea taarifa za hatua za Utekelezaji wa Bajeti (Planning, Budgeting and Reporting System- PlanRep) pamoja na Mfumo wa Kufanya Malipo na Kutoa Taarifa za fedha ambazo zimetumwa kwenye Vituo vya Kutoa Huduma (Facility Financial Accounting and Reporting System-FFARS).

Akiziungumza wakati wa sherehe za uziznduzi huo  Septemba 5, 2017 mjini Dodoma, Waziri Mkuu  amesema kuwa lengo la mifumo hiyo ni kuongeza uwajibikaji na ufanisi. Aidha, ameongeza kuwa mifumo hiyo iswe kikwazo katika utoaji wa huduma kwa jamii kwa jamii.  

Ameongeza kuwa mifumo hiyo imeshirikisha Wizara za Kisekta na Taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government Agency-eGA) kuanzia hatua za awali za ukusanyaji wa mahitaji hadi utengenezaji wa mifumo. Hii ni hatua kubwa sana katika utengenezaji wa mifumo muhimu kama hii.

“Napenda kuwafahamisha Viongozi na Watendaji wote kwamba, lengo la matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi na si kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za Serikali.” Amesema Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, kuwa mifumo hii ni muhimu sana kwa Taifa na inatakiwa itumike kwa ufasaha ili kuongeza tija inayotarajiwa na vilevile kila mmoja anawajibu wa kuilinda na kuitunza ili iweze kudumu na kuwa endelevu kwa manufaa ya Taifa.

“Ni matumaini yangu kuwa uwepo wa mifumo hii itawapa fursa viongozi wa mikoa na halmashauri na Vituo vya kutoa huduma za Elimu na Afya kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa mamlaka zinazohusika kwa wakati na bila kipingamizi” amesisisitiza Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa.            

Vilevile ameagiza viongozi na watendaji wote kwa ngazi zote za Mamlaka za Serikali za Mitaa zinato taarifa za mapato na matumizi kwa Wananchi wanaowahudumia kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na tovuti zilizozinduliwa mwezi machi 2017.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi Bw. George Simbachawene amesema mifumo hiyo itaziwezesha Halmashauri kupunguza gharama kubwa katika kukamilisha zoezi zima la uandaaji wa Mipango na Bajeti kwani zilikuwa zikitumia muda mrefu na gharama kubwa kwenye zoezi hilo.

“Hesabu za mwaka 2017/2018 zilizotolewa zinaonyesha kuwa gharama za mchakato wa maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya mwaka kwa Halmashauri 185 ni takriban sh. Bilioni 8.32 za kulipia usafiri (Mafuta), posho ya kujikimu, shajala na gharama za kudurufu Vitabu” amesema Mhe. Waziri Simbachawene.