emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Taasisi 72 Zaunganishwa katika Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali


Taasisi 72 Zaunganishwa katika Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali


Serikali imeunganisha Taasisi 72 katika Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali - (GovNet) kupitia Mkongo wa Taifa (NICTBB. Pia Taasisi 77 zilizo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI zitaunganishwa kwenye mtandao huo kufikia Disemba 2016. 

Hayo yamesemwa na Meneja Habari, Elimu na Mawasilano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto wakati wa kikao  na waandishi wa habari kilichofanyika Oktoba 20, 2016 katika ofisi za Wakala.

Bi. Mshakangoto amesema, taasisi hizo pia zimefungiwa Mtandao wa Ndani wa Mawasiliano (LAN) pamoja na mfumo wa simu zenye itifaki ya intaneti (IP). 

Aidha, amesema taasisi 72 zinajumuisha Wizara zote, Idara inazojitegemea ikiwemo Ofisi ya Bunge na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT) pamoja na Wakala za Serikali zikwemo Wakala ya Majengo Tanzania (TBA), Wakala wa Uzito na Vipimo (WMA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Utoaji Leseni  (BRELA). Pia, taasisi 77 kutoka mikoa 20 ya Tanzania Bara (Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Kagera, Lindi) ambapo kila mkoa unajumuisha ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Jiji. 

“Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaipunguzia Serikali gharama za mawasiliano, kutasaidia taasisi kuwa na mawasiliano bora ya kielektoni (data, sauti na video), kutaongeza kasi ya masafa ya intaneti, kutawezesha matumizi ya mifumo shirikishi ya TEHAMA, kutaboresha utendaji kazi na kuongeza ubora wa utoaji huduma kwa umma”, alifafanua Bi. Mshakangoto.

Ameongeza kuwa, taasisi zilizounganishwa na mfumo wa simu hizo zitaweza kuwasiliana baina yao  kwa urahisi. Mtumishi wa taasisi moja katika taasisi hizo anaweza kupiga simu kwenda taasisi nyingine ya nje ikawa kama amepiga simu ya ‘extension’ ndani ya ofisi moja. Mfumo huo wa simu pia unawezesha taasisi kufanya mikutano kwa njia ya simu, amesema Bi. Mshakangoto.

Katika kuhakikisha mtandao wa mawasiliano Serikalini pamoja na matumizi ya simu za IP zinakuwa zenye tija, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwa kushirikiana na Wakala imetoa Mafunzo kwa wataalamu wa TEHAMA na Makatibu Muhtasi kutoka Wizara, Taasisi Zinazojitegemea na  Wakala za Serikali zilizounganishwa  kuhusu  uendeshaji na usimamizi wa Mtandao wa Serikali na matumizi ya simu za IP.

Akizungumzia suala la usalama wa mawasiliano amesema, Wakala imejizatiti vya kutosha kwani kuna  kitengo maalum kinachoshughulikia masuala ya usalama wa mtandao na hivyo hakuna uwezekano wowote wa taarifa kutoka nje au kudukuliwa kupitia mifumo iliyopo.

“Kila taasisi ina namba ya pekee ya utambulisho ambayo haiingiliani na taasisi nyingine na orodha ya namba hizo inapatikana katika tovuti ya Wakala www.ega.go.tz eneo la machapisho na kurasa za karibu”, alisisitiza Bi. Mshakangoto.

Vilevile amesema ni mpango wa Serikali kufikia mikoa na halmashauri zote hapa nchini ili kutumia mawasiliano ya simu za itifaki, barua pepe na mifumo ya TEHAMA katika kubadilishana taarifa.