emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mhe. Celina Ompeshi Kombani Apumzishwa mjini Morogoro


Mhe. Celina Ompeshi Kombani Apumzishwa mjini Morogoro


Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambaye pia alikuwa Mbunge wa Ulanga Mashariki Mhe. Celina O. Kombani (Mb) umepumzishwa kwenye shamba lake lililopo Lukobe nje kidogo ya Mji wa Morogoro Septemba 29, 2015.

Maziko hayo yaliongozwa na Makamu wa Rais Mhe.Dkt.Gharib Bilal na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda na kuhudhuriwa na mke wa Rais mama Salma Kikwete, viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Wabunge, Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu , Manaibu Kabibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Watendaji Wakuu wa Serikali pamoja na mamia ya wananchi wa Mkoa huo.

Wakala ya Serikali Mtandao iliwakilishwa na Mtendaji Mkuu Dkt. Jabiri Bakari, Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa Huduma Bw. Ibrahim Mahumi, Mkurugenzi wa Udhibiti wa huduma za TEHAMA Bw. Michael Moshiro pamoja na Meneja wa Kitengo cha Rasilimali watu Bw. Lembris Laanyuni.

Wakati wa kuaga mwili wa Waziri huyo katika uwanja wa Jamhuri mjini humo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe. Jenister Mhagama amesema Serikali imepoteza kiongozi  mchapakazi na kamwe pengo lake haliwezi kuzibika.

Naye   Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jumanne Sagini amesema marehemu Kombani alikuwa  kiongozi aliyetekeleza majukumu yake kwa uadilifu na umakini mkubwa na alikuwa mlezi na mshauri kwa viongozi na watumishi wote wa TAMISEMI.

 Mhe. Kombani alifariki dunia Alhamisi ya septemba 24, 2015 katika Hospitali ya Indraprastha Appollo ya mjini Delhi, India alikokuwa amelazwa akitibiwa saratani ya kongosho. Mwenyezi MUNGU ailaze roho ya marehemu Celina Ompeshi Kombani mahali pema peponi, Amen.