emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Naibu Waziri Afurahishwa na Utendaji wa eGA


Naibu Waziri Afurahishwa na Utendaji wa eGA


“Nimeoneshwa mifumo madhubuti na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa ambayo imetengenezwa na Wakala ya Serikali Mtandao. Ukweli nimefurahishwa na jitihada zenu kama watumishi wa Umma na huu ndio uzalendo wa kweli ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli anasema kila siku. Hivyo, utamaduni huu uendelee na iwe ni sehemu ya msingi wa kazi zenu za kila siku”.

Maneno hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) alipofanya ziara katika ofisi ndogo za Wakala hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam.

Aidha, Naibu waziri huyo ameongeza kuwa misingi ya Utumishi wa Umma ni muhimu kuzingatiwa ili mipango na malengo yaliyowekwa na taasisi yakamilike kama ilivyopangwa.

“Zingatieni uzalendo, uadilifu, uaminifu, ubunifu na nidhamu ya kazi ili mifumo mnayotengeneza iwe yenye kurahisisha mwenendo wa utoaji huduma kwa umma…” amesisitiza Mhe. Naibu Waziri Dkt. Mwanjelwa.

Naibu Waziri huyo, amebainisha kuwa Shughuli zinazofanywa na Wakala ya Serikali Mtandao ndo mpango mzima kwa dunia ya sasa kwa kuwa unapofanya mambo kielektroni unarahisisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama, urasimu, kuokoa muda na kuziba mianya ya rushwa.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Kuwe Bakari amesema kuwa maendeleo ya Sayansi na Teknolojia Duniani yameifanya Wakala ya Serikali Mtandao kupambana kwa kiwango kikubwa ili kuwafikia waliotangulia kama vile Korea ya Kusini.

“Kuna hatua nne za ukuaji wa Serikali Mtandao, Tanzania inaendelea vizuri kwa kuwa  tuko hatua ya pili kuelekea ya tatu” amesema Dkt. Bakari

Dkt. Bakari amefafanua kuwa hatua ya pili inafikiwa pale mawasiliano kati ya Serikali na Wananchi, Serikali na Wafanyabiashara yanaposhamirishwa na mifumo tumizi inayowawezesha kuwasiliana na Serikali kwa baruapepe, uwezo wa kupakua fomu na nyaraka kwenye mtandao na kuzijaza na kuziwasilisha ofisini.

Hatua ya tatu nayo, ni pale ambapo wananchi wanapata huduma bila kutembelea ofisi za umma na kila kitu kinafanywa kwa simu au kompyuta yenye mtandao.

Aidha, Dkt Bakari ameongeza kuwa nchi kama Korea ya Kusini ambayo inafanya vizuri sana katika masuala ya Serikali Mtandao ina miaka zaidi ya thelathini katika jitihada hizi wakati Tanzania ina miaka sita tu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala Bw. Benedict Ndomba ameshukuru kwa ujio wa Naibu Waziri huyo na kuahidi kusimamia maelekezo aliyotoa na kuendelea kuhimiza watumishi kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na maadili ya utumishi wa umma wakati wote wa utendaji kazi.