emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Taasisi za Serikali zahimizwa kutumia teknolojia ya TEHAMA ili kuboresha huduma kwa umma.


Taasisi za Serikali zahimizwa kutumia teknolojia ya TEHAMA ili kuboresha huduma kwa umma.


Taasisi za Serikali nchini zimehimizwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutuoa huduma bora kwa umma. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue wakati akifungua Mkutano wa kwanza wa Serikali Mtandao uliofanyika Agosti 19, 2015, jijini Arusha.

Balozi Sefue amesema Serikali Mtandao siyo teknolojia pekee kama watu wengi wanavyoichukulia bali ni matumizi ya TEHAMA katika kuboresha utendaji kazi wa kila siku na pia alichukua fursa kuzipongeza taasisi za umma zinazochangia katika jitihada za kukuza Serikali Mtandao.

“Napenda kuzipongeza sana taasisi za umma ambazo zimefanikiwa kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma kwa umma kwa kutumia TEHAMA. Hivyo, taasisi za Serikali ambazo hazijaanza utekelezaji wa Serikali Mtandao, zinatakiwa kufahamu kuwa kuna mambo mawili, kubadilika au kubadilishwa” Alisema Balozi Sefue.

Balozi Sefue aliongeza kwa kusema kuwa mkutano huu utakuwa chachu ya kutoa msukumo mpya wa utekelezaji wa malengo ya Serikali Mtandao ikiwemo kujenga uwezo ndani ya Serikali na taasisi zake pia utekelezaji huu utasaidia Serikali kuendelea na awamu nyingine ya maboresho kupitia Programu ya Kuboresha Utumishi wa Umma (Public Service Reform Programme - PSRP) ambayo ilikusudia kuweka Mifumo ya Kusimamia Utendaji, kuboresha huduma zinazotolewa kwa umma na kujenga uwezo wa watumishi wake wa kutoa huduma hizo.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Kuwe Bakari amesema Mkutano huu ni wa kwanza kufanyika hapa Tanzania na anashukuru taasisi za umma kwa mwitikio mkubwa walioonyesha. Pia aliwakaribisha Dkt. Rajendra Kumar kutoka India pamoja na Bw.Tang Kim Leng kutoka Singapore ambao watabadilishana uzoefu wa nchi zao zinafanya vizuri katika TEHAMA.

Mkutano huo wenye kauli mbiu ‘‘Kuelekea Matumizi ya Rasilimali TEHAMA Zilizowianishwa katika kutoa Huduma Bora kwa Umma utasaidia  kuhamasishana, kukubaliana na hatimaye kuwa na uelewa wa pamoja miongoni mwa taasisi za umma katika kuhakisha kunakuwepo na uwekezaji wenye tija pamoja na usakinishaji wa miundombinu na mifumo ya TEHAMA.