emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Tovuti Kuu ya Serikali kuhuishwa


Tovuti Kuu ya Serikali  kuhuishwa


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao, Dr. Jabiri K. Bakari amewataka Maofisa Mawasiliano pamoja na TEHAMA wa taasisi za Serikali kuweka taarifa kwenye Tovuti Kuu ya Serikali ambazo zitawarahisishia wananchi kupata taarifa  mbalimbali na kujua shughuli zinazofanywa na Serikali yao.

Aliyasema hayo wakati akifungua rasmi mafunzo maalumu ya kuhuisha na kuweka taarifa mpya kwenye Tovuti kuu ya Serikali inayopatikana kwa anuani ya www.tanzania.go.tz kwa Maofisa kutoka taasisi zipatazo 30 zinazo shiriki mafunzo hayo, mafunzo hayo yanafanyika kwa muda wa siku tano (05) kuanzia tarehe 19-23 Oktoba, 2015 katika ukumbi wa mafunzo wa Wakala ya Serikali Mtandao jijini Dar-es-salaam.

“Asilimia hamsini ya taarifa kwenye Tovuti Kuu ya Serikali zinaonekana kuwa za muda mrefu na zimepitwa na wakati, hivyo mnatakiwa mfanye kazi ya kuzihuisha mara baada ya mafunzo haya” alisema Dr. Bakari.

Pia Dr.Bakari aliwashauri washiriki wa mafunzo hayo watumie fursa ya kuweka matangazo mbalimbali ya huduma zinazo tolewa na taasisi za Serikali kwenye Tovuti Kuu ya Serikali ili kupunguza gharama kwa Serikali zakwenda kutangaza kwenye vyombo vya habari mbalimbali.  

Tovuti Kuu ya Serikali ilitengenezwa  mwaka 2010 na kuzinduliwa rasmi Novemba 29, 2013 chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na imekuwa ni kitovu cha kutolea huduma mtandao zinazotolewa na taasisi za umma kwa wananchi, wafanyabiashara kwa haraka na urahisi.