emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi yapata Tovuti


Halmashauri ya Manispaa ya Moshi yapata Tovuti


Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imepata tovuti iliyotengenezwa kutokana na Mfumo wa Tovuti za Serikali (Government Website Framework) ambao ni mahususi kwa ajili ya Mikoa na Halmashauri.

Akizungumza wakati wa siku ya pili ya mafunzo yanayofanyika katika ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia Habari, Mawasiliano na Uhusiano Bw. Ramadhan Hamis amesema kuwa tovuti hiyo ni muhimu sana kwa ustawi wa wananchi wa Manispaa ya Moshi ambao kwa muda mrefu wamekuwa na kiu ya kupata huduma na taarifa za Manispaa kwa njia ya mtandao.

“Mimi binafsi ninapenda kushukuru uongozi wa Wakala ya Serikali Mtandao ambao bila hiyana umekubali kupokea barua yetu na kuleta wataalamu ambao wametupatia mafunzo thabiti na kuhakikisha tovuti ya Manispaa ya Moshi inatengenezwa na sisi wenyewe kutokana na ujuzi tuliopata” Alisema Bw. Ramadhani.

Aliogeza kuwa tovuti ni muhimu sana katika dunia hii ya sayansi na teknolojia kwa kuwa ni inatoa taarifa kwa umma na kuwapunguzia gharama, muda wa kupata taarifa za awali kuhusu huduma zinazotolewa na Manispaa.

Nae Ofisa Tehama wa Manispaa wa Moshi Bw. Robert Kwene amesema mfumo huu ni mzuri, rahisi na rafiki kwa waweka taarifa na hata kwa watumiaji. Vilevile kwa kuwa technolojia inabadilika mara kwa mara ni rahisi kufanya maboresho ya pamoja na kwa wakati mmoja.

“Ninamshukuru Mkurugenzi wetu wa manispaa Bw. Michael Mwandezi ambaye bila kusita amewaita wataalamu kutoka eGA ambao wametupatia mafunzo hayo muhimu ili pia manispaa yetu ipate tovuti yake na kufanana na manispaa nyingine Tanzania Bara” Alisema Bw. Kwene.

Mfunzo haya yametolewa kwa Ofisa Tehama na Mawasiliano wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia 19-21 Juni, 2017 baada ya kukosa mafunzo yaliyofanyika kwa pamoja katika mkoa wa Dodoma kuanzia tarehe 20 hadi 27 Machi 2017.

 

Uzinduzi wa Mfumo wa tovuti za Mikoa na Halmashauri ambapo Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa 185 ulifanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George Simbachawene (Mb) tarehe 27 Machi, 2017 huko mjini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtanda (eGA) Dkt. Jabiri Bakari na Mkurugenzi Msaidizi wa USAID Tanzania, Bw.Tim Donnay ambao ndio wafadhili wa Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).