emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wizara ya Afya Kushirikiana na Wakala


Wizara ya Afya Kushirikiana na Wakala


Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.Magret Mhando ameitaka Menejimenti ya Wizara hiyo kuendelea kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku ili kuweza kwenda pamoja na mabadiliko ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Dkt. Mhando amesema hayo kwenye kikao cha pamoja kati ya Wakala ya Serikali Mtandao na Menejimenti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Juni 09, 2015 katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo.

Aidha Dkt. Mhando ameiambia Menejimenti hiyo kuwa Wizara iangalie jinsi inavyotumia Serikali Mtandao katika utendaji kazi wake na muhimu kuwasiliana na eGA katika masuala mbalimbali yanahusu TEHAMA ili kuboresha ufanisi wa kazi.

“Kila mwaka Wizara itoe orodha ya miradi mbalimbali ya TEHAMA na kutafuta ushauri wa kitaalam kutoka Wakala ya Serikali Mtandao, pia Wizara iwe na mazoea ya kufanya mikutano kwa njia ya video (Video Conference) ili kupata taarifa kwa haraka”, alisema Dkt. Mhando.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala Bw. Benedict Ndomba amesema Wizara ya Afya ina mifumo mingi ambayo haiongei hivyo ni muhimu kuifanya mifumo hiyo iongee na kubadilishana taarifa ili kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha usalama wa taarifa za Serikali.

“Tutumie TEHAMA ili kuweza kuitumikia Umma kwa urahisi na ufanisi na kuwapatia huduma bora kwa wakati”, alisema Bw. Ndomba.

Wakala ya Serikali Mtandao inafanya vikao na Menejimenti za taasisi mbalimbali za umma ili kuweza kuitangaza Wakala pamoja na huduma zake.