emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Maofisa Habari na TEHAMA Waagizwa Kuhuisha Tovuti zao Kila Wiki


Maofisa Habari na TEHAMA Waagizwa Kuhuisha Tovuti zao Kila Wiki


Maofisa TEHAMA na Mawasiliano wameagizwa kuhakikisha kila mwisho wa wiki Tovuti zao zinakuwa na taarifa mpya. Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro,  Mhandisi Dkt. John Ndunguru ametoa agizo hilo wakati wa  ufunguzi wa Mafunzo kwa Maofisa Habari na TEHAMA wa Halmashauri na Mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Tanga  Machi 20, 2017 Mkoani Morogoro.

“Inapofika ijumaa Tovuti ya kila Halmashari na Mkoa inabidi iwe na taarifa mpya na ielezee shughuli zote zilizotendeka na taarifa nyingine yoyote ambayo wananchi wanahaki ya kuipata”, alisema Mhandisi Dkt. Ndunguru.

Vilevile Dkt. Ndunguru alisema kuwa moja ya haki ya kikatiba waliyonayo wananchi ni haki ya kupata taarifa, hivyo kwa kutokutoa taarifa zilizo sahihi na kwa wakati wananchi wanakuwa wamenyimwa na kukoseshwa haki yao ya kikatiba, hivyo kila ofisa aliyehudhuria mafunzo haya ahakikishe anawapa wananchi wake haki yao yakikatiba ya kupata taarifa. 

Aidha Katibu Tawala huyo alisisitiza kuwepo na ushirikiano baina ya Maofisa TEHAMA na Habari katika utendaji kazi wao wa kila siku na kufikia malengo yao ili kuweza kwenda sambamba na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu.

Awali akielezea mradi huo, Meneja Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) mkoa wa Morogoro, Bw. David Ole Laput amesema kuwa mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) ni wa miaka mitano, na utafanya kazi na Serikali Kuu pamoja na Halmashauri 93 katika mikoa 13 ya Tanzania bara ili kuboresha mawasiliano kwa umma. Pia kupitia mradi huo maofisa hao watajengewa uwezo wa kutengeneza tovuti, kuweka taarifa sahihi kwenye tovuti na kutangaza huduma mbalimbali wanazotoa kupitia tovuti hizo.

Mafunzo hayo ya wiki moja yanayoenda sambamba katika mikoa ya Dodoma, Mtwara,Kigoma na Mororgoro yatafikia kilele chake Machi 27, 2017 kwa uzinduzi rasmi wa Tovuti za  Halmashauri na Mikoa yote Tanzania bara.