emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Wekezeni katika Mifumo ya TEHAMA


Wekezeni katika Mifumo ya TEHAMA


 “Wekezeni, boresheni na ongezeni kasi katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuokoa muda na gharama za huduma na kufikia malengo mliyojiwekea kwa haraka zaidi”

Ushauri huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA), Dkt. Jabiri Kuwe Bakari wakati  akiwasilisha mada juu ya matumizi ya TEHAMA Serikalini wakati wa mafunzo ya utawala bora yaliyohusisha wajumbe wa bodi, wakurugenzi, wakuu wa idara pamoja na mameneja majengo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Dkt. Jabiri, amesisitiza kuwa mifumo ya TEHAMA inasidia katika mawasiliano na kupata uamuzi mapema. Hivyo,haina budi kutumia Tehama katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya taasisi muhimu kama hii. Aidha, amewashauri viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuboresha mifumo ya TEHAMA kwa kutumia watalaam wa Tehama wenye ujuzi wa kutosha na ambao wanaweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia hii ya Habari na Mawasiliano.

 “Tunatakiwa kutengeneza mifumo ya TEHAMA sisi wenyewe ili iwe rahisi kuboresha au kurekebisha pale inapotokea hitilafu. Utaratibu huu ni bora zaidi kuliko kununua mifumo ambayo imetengenezwa nje na hatujui imetumia au imetengenezwa kwa utaalam wa aina gani’’ amesema Dkt. Bakari.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa muda wa siku mbili na kuahirishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa hospitali hiyo Prof. Charles Majinge ambapo amewataka viongozi wa MNH kuzingatia mafunzo hayo ili kutekeleza vema majukumu yao kama watumishi wa Umma.

Washiriki wote wa mafunzo hayo walitunukiwa vyeti vya ushiriki kutoka Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT)