emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Ishirikisheni Wakala -Sefue


Ishirikisheni  Wakala -Sefue


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue ameziagiza taasisi zote za Umma kuishirikisha Wakala kila wanapobuni na kutekeleza miradi ya TEHAMA ili kuondoa urudufu wa miradi hiyo miongoni mwa taasisi hizo.

Balozi Sefue ameeleza hayo Agosti 19, 2015 jijini Arusha  alipokuwa akifungua Mkutano wa Kwanza wa Mwaka wa Serikali Mtandao kwa washiriki wa kundi la pili linalojumuisha Watendaji Wakuu wa taasisi za umma na viongozi wengine walio katika ngazi ya maamuzi.

Aidha, Sefue amezitaka taasisi hizo kutoa taarifa zote zinazohusu TEHAMA ili kuhakikisha Serikali inakuwa na taarifa zote zitakazosaidia katika kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya TEHAMA

Vilevile amezieleza taasisi hizo kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa kwa kuwa Serikali itajumuisha miongozo hiyo kama sehemu ya ukaguzi unaofanywa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.

“Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna sekta yoyote iliyoendelea bila kuratibiwa, kwa hiyo ni vema mkazingatia miongozo mbalimbali inayotolewa na Wakala katika kutekeleza Serikali Mtandao”, alisema Balozi Sefue.

Balozi Sefue amesisitiza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wakala ya Serikali Mtandao waendelee kushirikiana na Tume ya Mipango katika kuhakikisha masuala ya Serikali Mtandao yanaingizwa na kuoanishwa na Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano na mipango mingine ili kufikia malengo yaliyowekwa.

“Serikali imeweka mazingira mazuri ya kisera na kimkakati ili kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA yanakuwa na tija katika kuwahudumia wananchi na kuwaondolea kero mbalimbali na hivyo kufikia malengo ya kitaifa ya kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania”, alisema Balozi Sefue.

 Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Kuwe Bakari amesema dhima ya Mkutano huo ni kujenga uwezo na        ushirikiano katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma pamoja na kuwaleta pamoja wadau wakuu wa Serikali Mtandao  kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokabili utekelezaji wa Serikali Mtandao hapa nchini.

“Mkutano huu pia umelenga kuwawezesha washiriki kuongeza ufahamu, kubadilishana uzoefu, kushirikiana na kukuza uhusiano wa kikazi na wataalam wanaohusika na Serikali Mtandao kutoka nchi zinazofanya vizuri katika eneo la Serikali Mtandao hususani nchi za India na Singapore”alisema Dkt. Bakari.

Mkutano huo wa Serikali Mtandao ni wa kwanza kufanyika nchini ambapo zaidi  ya washiriki 700 kutoka taasisi za umma wamehudhuria wakiwemo Dr. Rajendra Kumar ambaye ni Ex-Joint Secretary (e-Gov), Department of Electronics and Information Technology, Government of India na Bw. TAN Kim Leng ambaye ni Managing Director, KDi Asia Pte Ltd kutoka Singapore.