emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wanahabari watakiwa kutumia fursa ya zabuni


Wanahabari watakiwa kutumia fursa ya zabuni


Wanahabari wametakiwa kuachana na dhana potofu kuwa zabuni inapotangazwa inakuwa imewalenga wale wenye uwezo kifedha bali waombe kwa ushindani ili kupata nafasi ya zabuni hiyo.

Hayo yamesemwa na Mtaalam wa masuala ya Zabuni kutoka Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Jones Mapunda alipokuwa akitoa mafunzo elekezi kwa wanahabari walioonesha nia ya kuomba zabuni ya kutengeneza vipindi vya kuelimisha umma kuhusu dhana ya Serikali Mtandao nchini kilichofanyika katika Ofisi za Wakala Disemba 14, 2015.

“Hakuna mtu yeyote  wala  chombo chochote cha habari kitakachopata zabuni hii kwa kuinunua bali tutazingatia vigezo vyote vilivyoainishwa kwenye nyaraka ya zabuni itakayotangazwa”, alisema Bw. Mapunda.

Aliongeza kuwa zabuni ilitangazwa kwa mara ya kwanza lakini ilionekana kuwa kuna udhaifu katika kujaza zabuni hiyo na hivyo kulazimika kukutana nao ili kuelimishana pamoja na kukubaliana kwenye vipengele vinavyoleta ukakasi kwenye nyaraka hiyo.

“Katika kikao hicho, tumekubaliana kuwa, upande wa Utayarishaji wa vipindi utagharimu asilimia sitini (60%) na muda wa kutangaza utapewa asilimia arobaini (40%) ya fedha zilizotengwa”, alisema Bw. Mapunda.

Naye Meneja wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto aliwataka waandishi hao kuisoma kwa makini na kuielewa zabuni hiyo ili wanapoomba wajue yale yaliyoandikwa kwenye zabuni hiyo.

Aidha, waandishi hao waliomba kupunguziwa idadi ya mikoa iliyopangwa kwa ajili ya kutengeneza vipindi hivyo na kuweka maeneo ya karibu, kwa kuwa umbali wa mikoa hiyo utaigharimu kampuni itakayoshinda zabuni na hivyo kufanya kazi kwa hasara.