emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Waziri Kairuki Ataka Mifumo Iongee


Waziri Kairuki Ataka Mifumo Iongee


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki ameitaka Wakala ya Serikali Mtandao kutengeneza mifumo itakayorahisisha utendaji kazi na kuipunguzia gharama Serikali. Pia, ameitaka Wakala hiyo kubuni mifumo itakayozungumza na kubadilishana taarifa na mifumo mingine ili iweze kurahisisha upatikanaji wa taarifa.

Mhe. Kairuki amesema hayo alipoitembelea Wakala na kufanya mazungumzo na watumishi wa Wakala hiyo Disemba 31, 2015.

“Yapo matatizo mbalimbali kama vile kughushi vyeti miongoni mwa watu wanaotafuta kazi na ulipaji mishahara hewa, hivyo tukiwa na Mifumo imara na inayozungumza itatusaidia kupambana na matatizo hayo”, alisema Mhe. Kairuki.

Aidha Mhe. Kairuki amesisitiza matumizi ya  Barua Pepe za Serikali na kuwataka watumishi wa Taasisi za umma kutumia barua pepe hizo katika masuala yote ya Serikali.

“Natoa siku 60 kwa watumishi wote wa Serikali kujiunga na kutumia barua pepe za Serikali kwa kuwa ni salama. Hatukatazi mtumishi kutumia anwani za barua pepe nyingine kwa matumizi binafsi ila kwa kazi za Serikali ni lazima barua pepe ya Serikali itumike”, alisisitiza.

Alisema, Wakala inatakiwa itumie wataalamu wa TEHAMA ili kuhakikisha kuwa thamani ya ununuzi na zabuni mbalimbali zinazotangazwa zilingane na huduma zinazotolewa. Pia, Ununuzi wa programu tumizi ufanyike kwa jumla, hivyo Wakala ya Serikali Mtandao pamoja na Wakala ya Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) wametakiwa kukaa pamoja na kuhakikisha kuwa suala hilo linafanyiwa kazi haraka.

Vilevile alisema,ni muhimu kuhakikisha kuwa mifumo ya serikali na huduma za Serikali zinapatikana kwa urahisi ili kuondokana na tatizo la mwananchi kufuata huduma anayoitaka kwenye taasisi ya umma bali atumie TEHAMA katika kuipata huduma hiyo.

Mhe. Kairuki alisema, suala la Usalama wa Mtandao lidhibitiwe na ameagiza Wakala kuwajengea uwezo watumishi wake ili waweze kutekeleza jambo hilo kwa ufanisi. Pia aliagiza Wakala iwajengee uwezo watumishi wa taasisi nyingine za umma ili waweze kuhuisha na kupandisha taarifa kwenye tovuti zao kwa wakati.