emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Maofisa Mawasiliano Watakiwa Kupandisha na Kuhuisha Taarifa


Maofisa Mawasiliano Watakiwa Kupandisha na Kuhuisha Taarifa


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt Jabiri Bakari amewataka maofisa mawasiliano Serikalini kuhuisha taarifa zilizopo kwenye tovuti za taasisi zao pamoja na tovuti Kuu ya Serikali kwa wakati ili mwananchi apate taarifa mpya na zinazoendana na wakati.

Dkt. Bakari amesema hayo Machi 14, 2016 katika kikao kazi cha Maofisa Mawasiliano Serikalini kilichofanyika katika ukumbi wa VETA mjini morogoro.

 “Ofisa Habari au Mawasiliano wa Serikali anatakiwa kuhakikisha tovuti inakuwa active muda wote kwa kupandisha na kuhuisha taarifa kwa muda mwafaka”, alisisitiza Dkt. Bakari

Aliongeza kuwa kazi kuu ya Wakala ya Serikali Mtandao katika tovuti hizo ni kuhakikisha matatizo yote ya kiufundi yanashughulikiwa pale yanapojitokeza.

Pia, alisema kuwa tovuti zote za Serikali zinatakiwa kutengenezwa kwa kufuata mwongozo wa Kusimamia na Kuendesha Tovuti za Serikali uliotolewa Disemba 2014 na aliwasihi kuusoma mwongozo huo unaopatikana kwenye tovuti ya Wakala kupitia www.ega.go.tz sehemu ya Miongozo na Viwango ili wapate kufahamu maudhui yaliyomo.

Vilevile alitoa wito kwa taasisi za Serikali kutumia kikoa cha .go.tz na kuachana na vikoa vingine ili pindi mwananchi anapoona tovuti yoyote yenye kikoa hicho ajue kuwa yupo kwenye tovuti ya Serikali na hivyo taarifa zilizopo ni za uhakika.

“Muda si mrefu tovuti za Serikali ambazo hazijasajili kikoa cha .go.tz hazitopatikana hewani ili kuwa na uwiano unaofanana”, alisisitiza Dkt. Bakari.

Kikao hicho kilianza Machi 14 hadi 18, 2016 na kilijumuisha maofisa Mawasiliano kutoka Serikali Kuu, Serikali za Mitaa pamoja na Taasisi nyingine za Umma nchini Tanzania.