emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Waziri Kairuki Aipongeza Wakala


Waziri Kairuki Aipongeza Wakala


Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki (mb) ameipongeza Wakala ya Serikali Mtandao (e-Government Agency) kwa ubunifu ilioufanya katika kutengeneza mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kazi ya kudhibiti matumizi ya TEHAMA Serikalini.

“Ubunifu na udhibiti wenu umeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha na kuongeza ubora na usalama wa mifumo,taarifa na vifaa vya TEHAMA vinavyotumika katika taasisi za Serikali. Kwa mfano, mfumo wa Barua Pepe uliobuniwa na kutengenezwa na Wakala na kuanza kutumika katika taasisi 66 umeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama kwa kuwa kama mfumo huo ungenunuliwa ungeigharimu Serikali kiasi kikubwa cha fedha”, alisema Mhe. Kairuki

Amesisitiza kwa kuziagiza taasisi zote za umma  kutumia barua pepe za Serikali na kuhakikisha kuwa kila mtumishi anatumia kwa ajili ya mawasiliano ya kiofisi.

Vilevile, ameagiza taasisi za umma kushirikiana na Wakala katika hatua zote za utekelezaji wa miradi ya TEHAMA hususan wakati wa kubuni na kutekeleza miradi ili Wakala iweze kutoa ushauri wa kitaalamu. Hatua hii itasaidia Serikali kuwa na miradi endelevu na ya gharama nafuu. Aidha, hatua hii itasaidia Serikali kuondokana na tatizo la kuwa na mifumo rudufu na isiyobadilishana taarifa.

Wakati huo huo, alisema anatarajia na ni mategemeo ya Serikali kuona mifumo ya RITA, NIDA, UTUMISHI, NECTA inakuwa na uwezo wa kubadilishana taarifa ili kuwa na chanzo kimoja chenye kuaminika cha taarifa muhimu za watu. Hatua hii itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo lililopo la baadhi ya watumishi kuwa na vyeti visivyo halali au mwananchi kuwa na taarifa zinazokinzana baina ya mifumo hiyo.

Aidha,  ameitaka Wakala kushirikiana na taasisi zote za umma hasa taasisi zinazosimamia Ununuzi wa Umma, zinaweka utaratibu wa ununuzi wa vianzi laini (Software) vya msingi vinavyotumika katika kuendesha Kompyuta za Serikali kwa pamoja “bulk procurement”  kwa kufuatana na bei ya soko, ili kupunguza gharama na kuongeza ubora katika vifaa vinavyonunuliwa.

Waziri huyo alisema kuwa anatambua kuwa moja ya majumu ya Wakala ni kuzisaidia taasisi za Serikali kuwa na Tovuti zao. Hivyo, ameiomba Wakala kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuzijengea uwezo taasisi nyingine za Serikali ili kuhakikisha kuwa taasisi hizo zinahuisha taarifa kwenye tovuti zao mara kwa mara.

Wakati huo huo aliongeza kuwa Serikali itaangalia uwezekano wa kuhuisha sheria, kanuni na Taratibu zinazosimamia Wakala ili iweze kuongeza ubunifu na udhibiti katika eneo hili na kuipa meno zaidi katika kusimamia matumizi stahiki ya TEHAMA Serikalini.