emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Naibu Waziri Azitaka Taasisi za Umma Kuzingatia Viwango na Miongozo ya Usalama wa Mifumo ya TEHAMA


Naibu Waziri Azitaka Taasisi za Umma Kuzingatia Viwango na Miongozo ya  Usalama wa Mifumo ya TEHAMA


“Naziagiza taasisi zote za umma kuzingatia viwango vyote vya usalama kwenye mifumo husika katika utekelezaji wa Serikali Mtandao. Usalama wa taarifa za Serikali liwe jambo la lazima wakati wa kubuni, kusanifu, kujenga, kusimika na kuendesha mifumoya TEHAMA, badala ya kujenga mfumo kwanza na unapokamilika ndipo masuala ya usalama wa mifumo ya TEHAMA yanafikiriwa”.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Pili cha Serikali Mtandao kwa kundi la Makatibu Wakuu na Maofisa Masuuli wa Serikali Kuu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano DODOMA Februari 1, 2019 

Dkt. Mwanjelwa amesema, tatizo la usalama mitandaoni linazidi kukua kadri maendeleo ya Teknolojia yanavyozidi kukua na hivyo, bila kukabiliwa kikamilifu, litaathiri kwa kiasi kikubwa jitihada zilizokwishafanyika katika eneo la Serikali Mtandao.

“Njia mojawapo ya kujihakikishia usalama, ni kuhakikisha utengenezaji wa mifumo yetu unazingatia programu ambazo watalaam wetu wanaweza wakatambua kinachofanyika badala ya kuwa na mifumo ambayo hatujui kinachoendelea nyuma ya pazia”,   amesisitiza Dkt. Mwanjelwa 

Vilevile, Dkt.Mwanjelwa amezitaka taasisi zote za Umma kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao iliyowekwa na inayoendelea kuwekwa ili kuhakikisha matumizi sahihi ya TEHAMA ndani ya Utumishi wa Umma. 

Pia, amezihimiza taasisi zote za Umma kushirikian naWakala kila zinapobuni na kutekeleza miradi ya TEHAMA ili kuondoa urudufu wa miradi ya TEHAMA miongoni mwa taasisi za Serikali. 

“Hatuwezi kuendelea kufanya kama tulivyofanya hapo awali kabla ya kuanzisha Wakala hii. Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna sekta yoyote iliyoendelea bila kuratibiwa, kwa hiyo ni vema mkazingatia miongozo mbalimbali inayotolewa katika kutekeleza Serikali Mtandao.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, iwapo utekelezaji wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA utawianishwa na kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa ndani ya taasisi za umma na baina ya taasisi za umma, utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao utakuwa ni  kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo ya viwanda. 

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari amesema dunia inahama kwa kasi kutoka  katika mfumo wa viwanda asilia vilivyotokana na mapinduzi ya viwanda (Industrial Revolution) ya Karne ya 18 kuelekea katika matumizi makubwa  ya TEHAMA ambayo yana mchango mkubwa katika kufikia Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda. 

“Hali hii inayojulikana kama mapinduzi ya Kidijitali (digital revolution) imetuingiza katika Zama za Taarifa (information Age) ambayo ni mhimili mkubwa katika maendeleo ya viwanda, na katika sekta zote (kilimo, Madni, Utalii, Elimu, Afya, Fedha, nk)”, amefafanua Dkt. Bakari.

Kikao  cha Pili cha Serikali Mtandao kimefanyika kuanzia Januari 30 hadi Februari 2, 2019 na kuhusisha zaidi ya watumishi wa umma 700 kutoka taasisi mbalimbali Serikalini