emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Taasisi za umma kuunganishwa kwa mtandao wa ndani (GovNet)


Taasisi za umma kuunganishwa kwa mtandao wa ndani (GovNet)


Serikali inaunganisha taasisi  za umma kwa mtandao wa ndani (GovNet) ili kuokoa gharama za mawasiliano zilizokuwa zinatolewa kwa ajili ya huduma ya mawasiliano baina ya taasisi moja ya umma na nyingine.

Hayo yamesemwa na Mkurungenzi Msaidizi wa Tehama Ofisi ya Rais Tamisemi Bw. Baltazar Kibola wakati akifungua mafunzo ya fibre optic cable kwa Maofisa Tehama wa Serikali kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa yanayofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Bw. Kibola alisema mafunzo haya ni ya awamu ya tatu na yanahusisha kuunganishwa Mikoa 20, Hospitali za Mikoa 19 na Mamlaka za Serikali za Mitaa 38 kwenye mtandao wa mawasiliano ya Serikali kwa teknolojia ya “fiber optics” kupitia mkongo wa Taifa, kuweka mitandao ya mawasiliano ya ndani (Local Area Network), usakinishaji wa mitambo ya kidigitali ya mawasiliano ya simu (IP PBX) pamoja na simu za digitali (IP Phones).

Aliongeza kuwa Mtandao huu wa Mawasiliano wa Serikali unafaida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji huduma kwa wananchi kwa jumla, kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa kurahisisha mawasiliano ya simu kati ya taasisi moja na nyingine.

Vile vile ni kuziwezesha taasisi za umma kufanya mikutano kwa njia ya mtandao (Video Conferencing/Teleconference), kubadilishana taarifa kwa urahisi, haraka na usalama, kuweka mazingira wezeshi na salama kwa ajili ya mifumo ya TEHAMA ya Serikali, kutumia miundombinu shirikishi ya TEHAMA kama vile mfumo wa barua pepe Serikalini (GMS), usimamizi rasilimali watu (HCMIS) na usimamizi wa fedha (IFMIS).

Katika utekelezaji wa mradi huu kwa awamu ya kwanza kazi mbalilimbali zilifanyika ikiwa ni pamoja na usakinishaji wa njia za mawasiliano ya Serikali kwa teknolojia ya “fiber optics” na usakinishaji wa vifaa vya mawasiliano kwenye taasisi za Serikali 72 ambazo ni Wizara 26, Idara za Serikali 17 na Wakala za Serikali 29.

Awamu ya pili ilihusisha usimikaji wa mitambo ya kidigitali ya mawasiliano ya simu (IP PBX) pamoja na simu za digitali (IP Phones), mtandao wa mawasiliano wa ndani (Local Area Network) na mitambo ya kuendesha mikutano kidigitali (Video Conference system) kwenye Tasisi za Serikali 72 ambazo ni Wizara 26, Idara za Serikali 17 na Wakala za Serikali 29.

Kwa  upande wake Mkurungenzi wa Taasisi inayojihusisha na kujenga Mtandao wa Mawasiliano  Kotes Tanzania Limited Bw. Max Komba alisema  wamejipanga  vizuri  kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Tehama juu  ya  kuendesha na kusimamia miundombinu hiyo kwa maofisa TEHEMA wa taasisi husika.

Alieleza kuwa  tangu kuanza kwa mradi huo hapa nchini Kotes imepata ushirikiano mkubwa toka Serikalini na malengo ya kampuni ni kukamilisha mradi huo nchi nzima kwa wakati uliopangwa.

“Miradi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni endelevu na inabadilika kila wakati hivyo msichoke kujifunza na kijiendeleza ili kufanya kazi kwa ufanisi”. alisema Bw. Komba.

Mtandao wa Mawasiliano ya Serikali ni mradi uliobuniwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kuunganisha na kuwezesha mawasiliano ya kielektroniki katika taasisi za Serikali ili kurahisisha na kupunguza gharama za mawasiliano na kuongeza ufanisi. Utekelezaji wa mradi huu unasimamiwa na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA).

Utekelezaji wa mradi huu unategemea kukamilika mwezi Desemba, 2016 na  unaenda sambamba na kujenga uwezo wa Wataalamu kwa kutoa mafunzo maalumu ya kitaalam ya jinsi ya  kuendesha na kusimamia miundombinu ya GOVNET kwa maofisa TEHEMA wa taasisi husika.