emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Sekta ya Afya Yatakiwa Kuzingatia Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao


Sekta ya Afya Yatakiwa Kuzingatia Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao


“Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni moja ya kiungo muhimu katika kurahisisha utendaji kazi na utoaii huduma kwa umma na hivyo wataalam wa TEHAMA hamna budi kuitumia ipasavyo na kuzingatia Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao vilivyowekwa ili kuongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wenu”.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Edward Mbanga alipofungua rasmi Kikao Kazi cha pamoja cha Wizara ya Afya na taasisi zilizopo chini yake kilichofanyika Dodoma Mei 23, 2019.

Aidha, Bw. Mbanga amesema kuwa Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa TEHAMA inakuwa chachu na kuleta tija na hivyo wataalam hao wa TEHAMA wanatakiwa kuitumia vile inavyotakikana ili kuboresha utoaji wa huduma ya sekta ya Afya nchini.

 “Tumekutana hapa ili kwa pamoja tuweze kupitia na kupata uelewa zaidi wa Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao ili kuhakikisha tunakuwa na matumizi sahihi ya TEHAMA katika kuendeleza kazi zetu za kila siku”.

Naye Meneja wa Usalama wa TEHAMA na Viwango kutoka Wakala ya Serikali Mtandao Mhandisi. Mosses Makoko amesema kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha matumizi ya TEHAMA pamoja na kuandaa Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao na hivyo wataalam wa TEHAMA wanatakiwa kujifunza na kuielewa Miongozo hiyo ili kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zao za kila siku.

“Ni wajibu wenu ninyi wataalam kuisoma na kuielewa kwa kina Miongozo na Viwango hivyo vinavyopatikana katika tovuti ya Wakala ya Serikali Mtandao sehemu ya Miongozo na Viwango https://www.ega.go.tz//standards. Kama mkikutana na changamoto yoyote, muwasiliane na Wakala ili muweze kupatiwa uelewa zaidi kuhusu Miongozo hiyo”, amesisitiza Bw. Makoko.

Akizungumzia umuhimu wa Kikao kazi hicho kwa wataalam wa TEHAMA, Bw. Makoko amesema kuwa mafunzo hayo yatawezesha huduma za Serikali Mtandao kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi kwa sababu matatizo kama vile urudufu wa mifumo, kuingia mikataba isiyo ya lazima na wakandarasi, pamoja na kila taasisi kujenga miundombinu yake badala ya kutumia miundombinu ya pamoja yatapungua.

“Elimu hii ya Miongozo na Viwango tunayoitoa eGA katika kikao kazi hiki ni yenye tija kwa sababu wataalam hawa wamekutana na kupata nafasi ya kujadiliana kwa pamoja changamoto na jinsi ya kuzitatua na hivyo natarajia kuwa baada ya kikao kazi hiki, wataenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia Miongozo na Viwango vilivyopo”, ameeleza Bw. Makoko.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Walter M. Ndesanjo amesema Kikao kazi hicho cha pamoja kina manufaa kwa kuwa Wizara na taasisi zake zimepata uelewa wa pamoja kuhusu Miongozo na Viwango jambo litakalosaidia kutumia TEHAMA kwa tija katika utoaji wa huduma za afya nchini.  

“Nawashauri wataalam wenzangu wa TEHAMA kutumia Miongozo na Viwango vilivyopo ili kuwa na matumizi ya TEHAMA yenye tija Serikalini ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi”, amesisitiza Bw. Ndesanjo.

Naye Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Afya Bi. Sultana Seiff amesema kupitia kikao kazi hicho amejifunza kuwa kama miongozo na viwango vitatumika kama inavyotakiwa, italeta mabadiliko chanya ikiwa ni pamoja na kuboresha utoaji huduma kwa umma na pia ameiomba eGA kutoa elimu hiyo kwa watendaji wengine Serikalini ili kuwa na uelewa wa pamoja.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Bohari ya Dawa Bw. Paschal Pastory amesema kikao kazi hicho kimemwongezea uelewa kuhusu miongozo na viwango vilivyopo jambo ambalo litaongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.

Kikao kazi hicho ni matokeo ya makubaliano yaliyotokea wakati wa Kikao Kazi cha Pili cha Serikali Mtandao 2019 ambapo Wizara na taasisi zake zilitakiwa kuandaa vikao kazi na kuialika Wakala ili kutoa elimu ya Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma.