emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Serikali Mtandao kukutanisha wataalamu wa TEHAMA


Serikali Mtandao kukutanisha wataalamu wa TEHAMA


 “Tunaandaa Kikao Kazi cha Pili cha Serikali Mtandao 2019 chenye lengo la kujenga uwezo, kuongeza ushirikiano na kuleta uelewa wa pamoja unaoziwezesha taasisi za umma kutoa huduma kwa kutumia  TEHAMA, kubadilishana uzoefu, kuendeleza uhusiano baina ya Serikali na wadau wa Serikali Mtandao na kujadili na kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini”.    

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari alipoongea na wadau wa Serikali Mtandao kuhusu kikao hicho hivi karibuni.

Vile vile amesema kuwa, Serikali imefanya jitihada nyingi katika utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini kama vile uunganishaji wa taasisi 149 katika mtandao mmoja wa mawasiliano Serikalini (GOVENET) kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, utengenezaji wa mifumo mbalimbali ya uboreshaji utendaji kazi Serikalini, utoaji wa huduma kwa umma na kurahisisha mifumo ya malipo Serikalini.

Dkt. Jabiri amesema pamoja na jitihada hizo, kuna changamoto nyingi zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa Serikali Mtandao, hivyo ni muhimu kwa wadau wote wa Serikali Mtandao kukutana na kujadili changamoto hizo na kuzifanyia ufumbuzi wakati wa kikao kazi hiki

Aidha,amefafanua zaidi kuwa, kikao kazi hicho cha pili cha Serikali Mtandao kitafanyika kwa siku 4 mfululizo kuanzia tarehe 30 Januari hadi tarehe 2 Februari, 2019 katika Ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano kilichopo Chuo Kikuu cha Dodoma.

Vilevile amesema washiriki zaidi ya 700 watahudhuria na watakuwa katika makundi matatu. Kundi la kwanza litakuwa tarehe 30 na 31 Januari, 2019 ambayo itawashirikisha Wakurugenzi wa TEHAMA, Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini, Maofisa Waandamizi wa TEHAMA, Maofisa TEHAMA na Watumiaji wa Mifumo (mf. Maofisa Habari, Biashara, Utumishi, Kilimo, n.k) na itafunguliwa rasmi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 

Kundi la Pili itakuwa tarehe 1 Februari, 2019 ambayo itawashirikisha Maofisa Masuuli wa Serikali Kuu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na itafunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Kundi la Tatu itakuwa tarehe 2 Februari, 2019 na itahusisha washiriki wote waliojisajili pamoja na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali kwa ajili ya Siku ya Utafiti na Ubunifu ya Serikali Mtandao ambayo itafunguliwa rasmi na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano (Mawasiliano). 

Dkt. Bakari ameongeza kuwa, Watafiti na Wabunifu watatakiwa kuwasilisha Andiko, Utafiti au Ubunifu unaolenga kuboresha huduma za Serikali kwa kutumia TEHAMA ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji

Kikao Kazi cha kwanza cha Serikali Mtandao kilifanyika mwaka 2015 jijini Arusha na kuhudhuriwa na washiriki takribani 700 kutoka taasisi mbalimbali za umma ambapo masuala mbalimbali ya TEHAMA yalijadiliwa.