emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Simu zinazotumia Itifaki ya Intaneti (IP phones) Kupunguza Gharama za Mawasiliano Serikalini


Simu zinazotumia Itifaki ya Intaneti (IP phones) Kupunguza Gharama za Mawasiliano Serikalini


Na Mambwana Jumbe

Simu ni chombo na nyenzo muhimu ya mawasiliano inayotumika kati ya mtu na mtu, mtu na kikundi cha watu ama kikundi kimoja cha watu na kikundi kingine. Kwa kufahamu umuhimu wa nyenzo hiyo, Serikali haiko nyuma katika kuhakikisha watumishi wake wanatumia kifaa hicho katika kufanikisha mawasiliano miongoni mwao na  umma kwa jumla.

Pamoja na  kufanikisha mawasiliano miongoni mwa taasisi za umma, simu  zimekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati muafaka na wananchi wamekuwa wakipiga simu na kutoa mapendekezo, kuomba ufafanuzi au kuomba huduma fulani kwa taasisi mbalimbali za umma na kupatiwa mrejesho wa jambo husika.

Mkurugenzi wa Miundombinu na Uendeshaji wa TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao, Bwana Benjamin Dotto anasema  moja ya mahitaji ya msingi kwa taasisi ya Serikali au nyingine yoyote,kuweza kutoa huduma kwa wananchi, ni uwepo wa mawasiliano baina ya wananchi na taasisi na baina ya taasisi na taasisi. Kuwezesha mawasiliano  imekuwa  changamoto ya muda mrefu kwa  Serikali na  inaendelea kufanyiwa kazi 

Mkurugenzi huyo anaelezea juhudi ambayo Serikali imefanya katika kutatua changamoto hiyo ni kuwapo kwa mtandao mmoja wa mawasiliano wa Serikali - Govnet ambapo Simu aina ya itifaki ya intaneti (Internet Protocol (IP) ambayo imeunganishwa na mtambo unaoitwa IP Private Branch Exchange (PBX) ndiyo zinazotumika kwa baadhi ya taasisi za Serikali zilizounganishwa kwenye mtandao huo.

Anaeleza kuwa, awali ili simu ziweze kufanya kazi katika utaratibu mzuri ulihitajika sana kuwapo kwa opereta wa simu anayesimamia swichibodi ili kuweza kuona simu inayotakiwa  kuingia ndani na ile inayotakiwa kutoka. Switchboard operators ndio walikuwa wakiunganisha simu kutoka nje kwenda ndani ya ofisi kwa kuunganisha kwenye saketi yenye mwito kutoka nje kuingia ndani naoperetahao walikuwa wakifanya kazikwa mkonoambapo mabadiliko ya teknolojia yamepelekea mfumo huo kupitwa na wakati

Anafafanua kuwa, kazi ya opereta ikapungua pale ilipoingia teknolojia mpya na mfumo mpya wa simu ulioitwa Private Branch Exchange (PBX) au Private Automatic Branch Exchange (PABX) kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya watu. Hii imesababisha kazi zote zilizokuwa zikifanywa kwa mikono kuwa otomatiki kwa asilimia kubwa na hivyo kazi nyingi zilizokuwa zikifanywa na swichibodi opereta zimekuwa rahisi kutokana na uwezo mkubwa wa mtambo huo.

Bw. Dotto anasema PBX ni mfumo wa simu unaowezesha mbadilishano wa mawasiliano ndani ya ofisi au kampuni. Pia huwezesha mawasiliano nje ya ofisi au kampuni, hivyo basi PBX ndio kitovu cha mawasiliano yote ndani na nje ya ofisi. Anasema, simu zote ndani ya ofisi huunganishwa kijanibu (locally connected) ambapo kila simu inaunganishiwa mkondo (extention) na hupewa namba yake husika, kwa hiyo, mawasiliano yote ndani ya ofisi yanakuwa hayana gharama (extention to extention call) kwani simu zote zimeunganishwa kijanibu (locally connected) kwenye mtambo mmoja ndani ya ofisi.

Anafafanua kuwa, kutokana na mabadiliko ya teknolojia kumesababisha mfumo wa PBX ambao mara nyingi umekuwa ukitumia teknolojia ya analojia (ambao unasafirisha taarifa kupitia electric pulses) kupitwa na wakati na hivyo kuhamia kwenye teknolojia ya kidijitali ambayo inaruhusu usafirishaji wa taarifa kupitia tendo cheuzi- binary format (zero and ones).

Mkurugenzi Dottto anasema, mfumo wa kidijiti umepata nguvu na matumizi yake yanaongezeka pia kwa kuwapo kwa teknolojia ya kompyuta ambayo inatambua ishara za kidijitali. Leo digital computer and communication technology imebadilisha kila kitu katika sekta ya mawasiliano kwa uwapo wa kompyuta, simu za mkononi na intaneti.

Kwa upande wa IP PBX anasema, huo ni mfumo wa simu unaofanya kazi kwenye mtandao ambao unaotumia itifaki ya intaneti (IP Protocol) kwa ajili ya mawasiliano kutoka sehemu moja hadi nyingine. Mtandao unaotumia IP ndio mtandao unaotumiwa na kompyuta kwa mawasiliano ndani na nje ya ofisi kupitia intaneti na mfumo huo wa IP-PBX unafanya kazi pamoja na IP Phones unaunganishwa na IP PBX kupitia mtandao wa itifaki ya intaneti (IP Network).

Vilevile anasema, sifa nyingi za PBX zimeendelea kuwapo pia katika IP PBX na zinaboreshwa zaidi kwa kuwa kupitia mtandao huo wa itifaki ya intaneti mambo yanafanyika kiurahisi kama vile uwapo wa  mawasiliano ya video na sauti au ujumbe mfupi wa papo kwa papo.

Hivyo, kutumika kwa mtandao wa itifaki ya intaneti katika mawasiliano ya simu kunawezesha mawasiliano ndani ya ofisi kupitia mitandao ileile inayotumiwa na kompyuta lakini pia inawezesha mawasilano kati ya ofisi na ofisi kama vile ofisi moja kwenda ofisi nyingine iwapo ofisi hizo zimeunganishwa kwenye mtandao mmoja wa itifaki ya mtandao wa intaneti.

Naye Meneja wa Kitengo cha Mtandao wa Mawasiliano Serikalini - Govnet wa Wakala Bw. Ricco Boma anasema Wakala ya Serikali Mtandao imefunga mitambo  ya IP PBX na IP Phones katikaa taasisi 72 za Serikali zikiwemo Wizara, Idara zinazojitegemea pamoja na Wakala za Serikali (MDAs)ikiwa ni njia mojawapo ya kuhakikisha mawasiliano yaliyo bora na salama kwa taasisi za Serikali na hivyo kuipunguzia gharama Serikali kwa jumla. 

Hata hivyo, mawasiliano kati ya taasisi iliyopo ndani ya mtandao wa Serikali na ile iliyopo nje ya mtandao yanawezekana kupitia kwa mtoa huduma ya simu za mezani  (PSTN provider) kama vile TTCL.

Akifafanua kuhusu manufaa ya simu hizo, Bw. Ricco anasema simu hizo, zinasaidia taasisi za Umma kuwa na mawasiliano yaliyo salama. Kuwa salama maana yake ni taasisi za umma zinabadilishana taarifa kupitia mtandao mmoja tu wa mawasiliano wa Serikali. “IP PBX”na “IP Phones”- aina ya simu ambazo zina uwezo mkubwa na ubora wa mawasiliano na kwa kuwa zinapitia kwenye mfumo wa Serikali hazina gharama za ziada.

Anasema simu aina ya IP ambazo zinatumia intaneti kwa kiasi kikubwa zimeipunguzia gharama Serikali kwa kuwa zinatumia miundombinu ya Mtandao wa Serikali ambapo mtumishi wa taasisi moja ya umma anaweza kupiga simu kwenda taasisi nyingine kwa kutumia extention bila gharama yoyote tofauti na hali ilivyokuwa  awali. Pia, gharama za simu kwa taasisi zinapungua kwa kuwa zinatumia miundombinu ya Govnet kwa kuacha kutumia huduma za makampuni makubwa ya mawasiliano.

Manufaa  mengine kwa mujibu wa Bwana Boma ni, kwamba kwa kutumia simu hizo, watumishi wanaweza kuwasiliana kupitia call conference ambayo imefungwa na PBX. Hivyo watumishi wanaweza kufanya vikao ndani na nje ya ofisi ili mradi wawe wmeunganishwa kwenye mtandao mmoja wa mawasiliano kupitia mtandao wa mawasiliano wa itifaki ya intaneti yaani IP Network.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Bakari anasema unganishaji wa simu hizo, umefanywa kutokana na utekelezaji wa  Mradi wa Mawasiliano ya Serikali ambapo Wakala iliziunganisha taasisi  72 zikiwemo Wizara, Idara zinazojitegemea pamoja na Wakala za Serikali (MDAs) 

Ni dhahiri kuwa uwepo wa mitambo ya PBX na simu aina ya IP zilizounganishwa kwenye Mtandao mmoja wa Mawasiliano Serikalini-Govnet, unaiweka  Serikali na taasisi zake katika mazingira yaliyo salama na uhakika kwa kuwa mawasiliano yameboreshwa na bila shaka kasi ya utoaji, utendaji na ubadilishanaji wa taarifa pamoja na utoaji huduma kwa umma itaongezeka maradufu.