emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TIO Wapata Mafunzo


TIO Wapata Mafunzo


Wakala ya Serikali Mtandao inaendesha mafunzo ya jinsi ya kuandaa na kuweka taarifa katika tovuti ya ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO) baada ya kutoa huduma ya kusanifu na kutengeneza tovuti hiyo inayopatikana kwa anuani ya www.tio.go.tz

Akifungua mafunzo hayo, ofisa TEHAMA wa Wakala Bw. Bernard Amri alisema  mafunzo hayo yatawasaidia maofisa kuandaa na kuweka taarifa katika tovuti hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wakala ya Serikali Mtandao katika kuhakikisha taasisi za umma zinatoa taarifa mbalimbali kwa urahisi,haraka na gharama nafuu.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Ofisa Mwandamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala kutoka ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro Bw.Osward Samki amesema kuwa, ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro itatumia fursa hii katika utoaji wa elimu kuhusu shughuli zinazofanywa na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na hivyo wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati.

Aidha, alisema kuwa Wakala inafanya kazi kubwa ya kuziwezesha taasisi za umma jambo linalopelekea taasisi hizo kuweza kutoa taarifa kwa wananchi wanaowahudumia kwa haraka.

“Nawapongeza sana kwani sasa wananchi wananufaika kwa kupata taarifa za Serikali na huduma zinazotolewa na taasisi husika kupitia tovuti. Naamini wananchi watanufaika na uwapo wa tovuti yetu”, alisema Bw. Samki.

Wakala imekuwa ikisanifu na kutengeneza tovuti mbalimbali za Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa umma. Pia imekuwa ikiendesha mafunzo ili kuwajengea uwezo na ujuzi maafisa mbalimbali katika kuandaa, kuhuisha na kupandisha taarifa mbalimbali za taasisi kwa ajili ya tovuti zao. Mafunzo hayo yanafanyika katika ofisi za Wakala kwa muda wa siku tatu kuanzia Februari 8 hadi 10, 2016.