emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma

Taasisi za Umma Zashauriwa Kuweka Taarifa za Miradi Ya TEHAMA Kwenye Mfumo wa Serikali wa kusimamia Miradi (GIP)


Taasisi za Umma Zashauriwa Kuweka Taarifa za Miradi Ya TEHAMA Kwenye Mfumo wa  Serikali wa kusimamia Miradi (GIP)


Mkuu wa sehemu ya Usimamizi wa Miradi na Programu za Serikali Mtandao Bw. Nassor Laizer amezishauri taasisi za umma kuweka taarifa za miradi yao ya TEHAMA iliyopo kwenye mipango, miradi  inayoendelea na iliyokamilika kwenye Mfumo wa  Ukusanyaji wa Taarifa za Miradi na Rasilimali za TEHAMA Serikalini (GIP) unaopatikana kupitia https://gip.gov.go.tz/

Ushauri huo umetolewa wakati wa kikao cha pamoja na wataalam wa TEHAMA kutoka Wakala ya Serikali Mtandao na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na taasisi zake kilichofanyika Dodoma hivi karibuni. 

Ameongeza kuwa, ‘GIP’ ni zana kuu ya kukusanya na kusimamia taarifa kuhusu miradi ya TEHAMA, mifumo, miundombinu na taarifa za TEHAMA za kitaasisi ambao unasaidia katika kuimarisha uwazi wa utekelezaji wa Serikali Mtandao kwenye taasisi za umma na kupunguza urudufu wa juhudi za Serikali Mtandao na kusaidia utumiaji wa rasilimali shirikishi.

“ Mfumo huu wa ‘GIP’ ni hazinadata ya pamoja ya jitihada za Serikali Mtandao na taarifa za miradi zikiwekwa kwa usahihi inakuwa rahisi kuona na kupima  malengo yaliyokusudiwa kwa kuwa miradi hiyo itawekwa kwenye mpango wa utekelezaji na hivyo usimamizi, ufuatiliaji na udhibiti wake unakuwa rahisi, Pia itairahisishia Serikali kufanya uamuzi sahihi kuhusu miradi hiyo”. Ameeleza Bw. Laizer. 

Aidha Bw. Laizer amesema, miradi mingi imekuwa ikishindwa kufikia malengo kwa sababu ya kutokuwa na udhibiti wa viwango na mikakati imara na endelevu ya kuhakikisha matokeo ya miradi hiyo yanakuwa chanya. 

Vilevile amesema, taasisi za umma zinapaswa kuweka taarifa za rasilimali watu, vianzi laini na rasilimali nyingine muhimu zitakazosaidia uendeshaji wa programu mbalimbali za Serikali mtandao kwa ufanisi na tija.

Naye Kaimu Mkurugenzi kutoka Bohari ya Dawa Bw. Paschal Pastory amezishauri taasisi za umma ambazo bado hazijaweka taarifa zao za Miradi ya TEHAMA kuziweka kwenye mfumo wa GIP ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Kwa kweli naipongeza eGA kuja na mfumo huu wa GIP kwa kuwa ni mfumo mzuri na tumekuwa tukiona matokeo ya miradi mbalimbali na kwa sasa suala la miradi kusuasua na kutofikia mwisho  halipo tena”, amesema Bw. Pastory.