emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Institutions get website training


Institutions get website training


Wakala ya Serikali Mtandao imewapatia mafunzo ya namna ya kuandaa na kuweka taarifa katika tovuti za Makumbusho ya Taifa na taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania baada ya kutoa huduma ya kusanifu na kutengeneza tovuti hizo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhandisi wa Sauti kutoka Makumbusho ya Taifa, Sixmund J. Begashe amesema  tovuti yao, inayopatikana kwa anuani www.museum.go.tz itawaleta karibu na wadau wao mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania kwa kuwa taarifa zote muhimu zinazohusiana na Makumbusho ya Taifa, zitapatikana kwa lugha mbili yaani Kiswahili na Kiingereza.

“Tunaishukuru Wakala ya Serikali Mtandao kwa kututengenezea tovuti yetu kwa lugha mbili ambazo zinakidhi haja ya wadau wetu. Pia, kupitia tovuti hii mwananchi atafahamu majukumu yetu, huduma tunazotoa pamoja, historia yetu na mambo kadha wa kadha”, alisema Bw. Begashe.

Naye Bw. Godson  Basinda ambaye ni Mtafiti kutoka Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) amesema kwa kutumia tovuti yao, inayopatikana kwa anuani www.tosci.go.tz wadau wao watapata taarifa mbalimbali zinazohusu taasisi hiyo.

“Tovuti hii itatuweka karibu na wadau wetu na itatufanya tufahamike na watu mbalimbali. Pia, kwa kuwa tovuti hii itakuwa kiungo na mfumo wetu wa TOSCI, itasaidia sana kutoa huduma kwa njia ya mtandao kwa sababu mdau ataweza kupakua fomu anayoitaka na kuituma moja kwa moja kupitia mtandao”, alisisitiza Bw. Basinda.

Wakala imekuwa ikiendesha mafunzo ili kuwajengea uwezo na ujuzi maafisa mbalimbali katika kuandaa, kuhuisha na kupandisha taarifa mbalimbali za taasisi kwa ajili ya tovuti zao. Mafunzo hayo yanafanyika katika ofisi za Wakala kuanzia Julai 10 hadi 14, 2017.