emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Watumishi wa Wakala Watakiwa Kuzingatia Uweledi


Watumishi wa Wakala Watakiwa Kuzingatia Uweledi


Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) wametakiwa kufanya kazi kwa uweledi ili kuzitumikia taasisi za Umma na Watanzania kwa jumla kwa ufanisi, haraka na gharama nafuu.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mstaafu) Mhe. George Mkuchika alipotembelea Ofisi za eGA kwenye jengo la TTCL Oktoba 17, 2017 kwa lengo la kufahamu shughuli zinazofanywa na eGA ikiwa ni moja ya taasisi zilizo chini ya wizara yake.

 “Watumishi wa eGA na Wizara kwa jumla ni kioo cha Serikali kwa sababu mnawatumikia watumishi wa Serikali na umma  kwa hiyo zingatieni uweledi, mfanye kazi kwa kadiri ya majukumu ya kazi ya kila mmoja wenu bila ya upendeleo au kubaguana na muwe na ushirikiano” , alisema Waziri Mkuchika.

Kuhusu changamoto za rasilimali fedha na watu, Waziri Mkuchika amesema Serikali itazifanyia kazi kwani kazi inayofanywa na eGA ya kuhudumia taasisi zote za Serikali ni kubwa na inahitaji wataalamu wa kutosha na kuipongeza eGA kwa kazi nzuri inayofanya.

Aidha Waziri huyo amesema kuwa jitihada za Serikali Mtandao na matumizi ya TEHAMA yamesaidia sana kupunguza muda na gharama katika ukusanyaji mapato na kutoa mfano wa jimbo lake la uchaguzi la Newala ambapo mapato yameongezeka mara nne.

Vilevile Waziri Mkuchika amepongeza huduma mbalimbali za Serikali Mtandao na kusema kuna haja ya kuongeza kasi zaidi ili mifumo yote ya taasisi za Serikali iweze kuwasiliana na ifike wakati mtu akienda kuomba pasi ya kusafiria mifumo ya Idara ya Uhamiaji iweze kupata taarifa za mwombaji kwenye mifumo ya Wakala ya Vitambulisho ya Taifa (NIDA) pamoja na Wakala ya Usajili wa Ufilisi, Udhamini na Vifo (RITA).

Akishukuru kwa niaba ya wafanyakazi wa eGA, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala, Bw.Benedict Ndomba amesema kuwa ujio huo umewapa ari mpya ya kufanya kazi kwa bidii zaidi na kuahidi kutekeleza maelekezo yote yatolewayo na Serikali kupitia Waziri huyo.