emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

eGA na TCRA Zatoa Elimu ya kusimamia usalama wa mifumo ya TEHAMA Serikalini


eGA na TCRA Zatoa Elimu ya kusimamia usalama wa mifumo ya TEHAMA Serikalini


Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Maria Sasabo amesema kuwa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wamejipanga na wapo tayari kutoa huduma za elimu kuhusu kinga (assessment), namna ya kufanya tathmini, kupima uhimilivu wa mifumo, kupendekeza teknolojia sahihi pasipo na gharama kwa taasisi

Dkt. Maria Sasabo amesema hayo alipofungua mafunzo ya awali ya kusimamia usalama wa mifumo ya TEHAMA Serikalini yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma Julai 12, 2019.

Vilevile amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia katika kujenga maadili katika kulinda na kutuma taarifa muhimu, kukinga taarifa zisitumike bila idhini, kulinda taswira na kupunguza gharama za mtumiaji au hasara zinazoweza kutokea kutokana na matumzi yasiyo salama ya mtandao.

Aidha, Dkt. Sasabo amesema Serikali imefanya juhudi kubwa na kutoa kipaumbele kwa kuweka mazingira imara ya matumizi ya TEHAMA kama vile kuwa na Sera ya TEHAMA ambayo ili kwenda na kasi ya mabadiliko ya TEHAMA ilihuishwa mwaka 2016, Kuwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA, Kuwa na Wakala ya Serikali Mtandao ili kuhimiza na kusimamia matumizi ya TEHAMA Serikalini na kuwa na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

“Juhudi nyingine ni kuwa na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sheria ya Mfuko wa Fursa za Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kuwa na taasisi na vitengo mahsusi kusimamia usalama wa mtandao ikiwa na pamoja na Computer Emergence Response Team (TZ-CERT) ambayo huratibu matukio ya viashiria hatarishi katika usalama wa mtandao kitaifa na kushirikiana na taasisi za kimataifa kupata utatuzi wa kuondoa vihatarishi vya usalama wa mtandao”, amefafanua Dkt. Sasabo.

Vilevile, Dkt. Sasabo ameipongeza Wakala ya Serikali Mtandao na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ambazo ni mihimili ya maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini hususani katika kulinda haki na usalama wa wananchi na rasilimali zao katika matumizi ya mtandao.

Naye Meneja wa Usalama wa TEHAMA na Viwango kutoka Wakala ya Serikali Mtandao Mhandisi. Mosses Makoko amesema kuwa Serikali imeandaa Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao ambavyo vinatakiwa kufuatwa na kuzingatiwa na wataalamu wa TEHAMA katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Lengo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na usalama na usiri kwenye matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuongeza tija, ufanisi na uwajibikji katika utoaji wa huduma kwa umma.

“Ninyi ndio mabalozi wetu kwa hiyo elimu hii mliyoipata hapa mnatakiwa muipeleke kwenye taasisi zenui ili tuweze kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu usalama wa mtandao. Pia tembeleeni tovuti ya Wakala sehemu ya Miongozo na Viwango https://www.ega.go.tz//standards ili muone na mpate maelezo ya kina kuhusu Miongozo na Viwavyo vya Serikali Mtandao vilivyopo kwa kuwa ninyi kama wataalam wa TEHAMA hamna budi kuisoma na kuielewa inavyopaswa”, anasisitiza Mhandisi Makoko.

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao na yamehudhuriwa wataalamu wa Teknoloji ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka taasisi 43 za Serikali.